Kimataifa

Trump kifua mbele kura zikihesabiwa Amerika, Harris aambia wafuasi waende nyumbani

Na BENSON MATHEKA NA MASHIRIKA November 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

DONALD Trump wa chama cha Republican alikuwa kifua mbele katika uchaguzi wa urais Amerika uliofanyika Jumanne, akionekana kuungwa mkono zaidi kuliko alivyokuwa katika kampeni zake ambazo hazikufanikiwa mwaka 2020, ingawa matokeo yalibakia kutofahamika katika majimbo yenye ushindani mkali ambayo yataamua mshindi.

Trump, akiwania kuwa rais wa kwanza wa zamani kurejea Ikulu ya White House katika zaidi ya miaka 100, alikuwa ameshinda kura 230 zinazoamua mshindi ikilinganishwa na 210 za mpinzani wake wa chama cha Democratic, Makamu wa Rais Kamala Harris, huku thuluthi moja ya kura zikiwa zimehesabiwa.

Huku Trump akishikilia uongozi katika majimbo  muhimu ya Georgia na Carolina Kaskazini, njia ya wazi ya Harris ya ushindi ilibaki Michigan, Pennsylvania na Wisconsin. Mgombeaji anahitaji jumla ya kura 270 kati ya 538, jimbo kwa jimbo ili kugombea urais.

Trump alipata uungwaji mkono zaidi katika kura za maoni kutoka kwa Wahispania, wapiga kura wa jadi wa Democratic, na familia zenye mapato ya chini ambazo zimehisi kupanda kwa bei tangu uchaguzi uliopita wa rais mnamo 2020.

Trump alishinda asilimia 45 ya wapiga kura wa Uhispania kote nchini, akimfuata Harris aliyezoa asilimia 53.

Lakini ni majimbo saba ya Arizona, Georgia, Michigan, Nevada, North Carolina, Pennsylvania na Wisconsin ambayo yataamua atakayetangazwa mshindi.