Kimataifa

Uamuzi wa kihistoria dunia ikisubiri kitakachotokea Amerika

Na BENSON MATHEKA, REUTERS November 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

BAADA ya kampeni kali za uchaguzi wa urais, Amerika itaandikisha historia kwa kuchagua mwanamke wa kwanza kuwa rais au kurudisha rais aliyeondoka mamlakani katika Ikulu ya White House akiwa amehukumiwa na Mahakama.

Iwapo Donald Trump wa chama cha Republican ataibuka mshindi, itakuwa mara ya kwanza kwa rais wa zamani kurudi mamlakani Amerika baada ya muhula mmoja. Na Kamala Harris wa chama cha Democratic akishinda, atakuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa nchi hiyo yenye uwezo mkubwa ulimwenguni.

Trump alishindwa na Joe Biden miaka minne iliyopita baada ya kuhudumu kama rais kwa muhula mmoja akashtakiwa kwa makosa yaliyohusisha kutoa hongo kuficha ukweli na kupatikana na hatia.

Hata hivyo, baada ya kupigana mahakamani, hukumu yake ilisitishwa hadi baada uchaguzi na pengine baada ya kuondoka mamlakani iwapo atatangazwa mshindi wa uchaguzi wa jana.

Wakati wa kampeni, Trump alinusurika majaribio mawili ya kumuua naye Harris alipata tiketi ya chama cha Democratic ghafla baada ya Rais Joe Biden kujiondoa uchaguzini.

Kura za kwanza zilizopigwa siku ya uchaguzi ziliakisi mgawanyiko katika nchi nzima wagombeaji wawili hao wakionekana kutoana jasho katika majimbo muhimu. Wapiga kura sita waliojiandikisha katika kitongoji kidogo cha Dixville Notch, New Hampshire, waligawa kura zao kati ya Harris na Trump baada ya saa sita usiku.

Kwingineko katika Pwani ya Mashariki, kura zilianza kupigwa saa moja asubuhi saa za Amerika katika majimbo zaidi ya kumi na mawili.

Waamerika wapanga foleni kupiga kura katika uchaguzi mkuu Novemba 5, 2024. Picha|Reuters

Afisi ya kampeni za Trump ilidokeza kuwa angejitangaza mshindi usiku wa uchaguzi mamilioni ya kura bado zikiwa zinahesabiwa, kama alivyofanya miaka minne iliyopita.

Rais huyo wa zamani amekuwa akisema mara kwa mara kushindwa kwa aina yoyote kunaweza tu kutokana na ulaghai mkubwa, akirejelea madai yake ya uwongo aliyotoa 2020. Huenda mshindi asijulikane kwa siku kadhaa ikiwa tofauti katika majimbo muhimu ni ndogo kama inavyotarajiwa.

Hata hivyo, bila kujali nani atashinda na kuingia ikulu ya White House, historia itawekwa Amerika.

Harris, 60, makamu wa rais wa kwanza mwanamke, atakuwa mwanamke wa kwanza, mwanamke mwenye asili ya Kiafrika na Mweusi na Amerika Kusini kushinda urais. Trump, 78, rais pekee kushtakiwa mara mbili na rais wa kwanza wa zamani kuhukumiwa kwa makosa ya jinai, pia atakuwa rais wa kwanza kushinda mihula isiyofuatana katika zaidi ya karne moja.

Kura za maoni katika siku za mwisho za kampeni zilionyesha wagombeaji hao wakigawa kura kila majimbo saba ambayo yana uwezekano wa kubaini mshindi: Arizona, Georgia, Michigan, Nevada, North Carolina, Pennsylvania na Wisconsin.

Kura za Reuters/Ipsos zinaonyesha pengo kubwa la kijinsia, huku Harris akiongoza miongoni mwa wanawake kwa asilimia 12 na Trump akiwa kifua mbele kati ya wanaume kwa asilimia 7.

Matokeo haya yanaonyesha taifa lenye mgawanyiko mkubwa ambao umeongezeka zaidi wakati wa kampeni zenye ushindani mkali.

Trump ametumia maneno makali kwenye kampeni. Harris aliwataka Wamarekani kuungana, huku pia akionya kwamba muhula wa pili wa Trump utatishia misingi ya demokrasia ya nchi yao. Udhibiti wa mabunge yote mawili ya Congress pia unamenyaniwa.

Wanachama wa Republikan wana uwezo wa kuthibiti Seneti ya Amerika, ambapo wale wa Democratic wanatetea viti kadhaa katika majimbo yanayoegemea upande wa Republican, huku Bunge la Wawakilishi likionekana kuwa wazi kwa chama chochote.

Wagombeaji hao walitumia wikendi ya mwisho katika majimbo yanayoweza kuegemea upande wowote. Trump alifanya mkutano wake wa mwisho Jumatatu jioni huko Grand Rapids, Michigan na Harris akafanya mikutano miwili huko Pittsburgh na Philadelphia.

Zaidi ya Wamarekani 80 milioni walikuwa tayari wamepiga kura kabla ya Jumanne, kupitia barua au kujitokeza kibinafsi vituoni, kulingana na kituo cha kufuatilia chaguzi Chuo Kikuu cha Florida Election Lab.

Wakati wa kampeni, Trump kwanza alimponda Biden na kisha Harris kuhusiana na masuala ya kushughulikia uchumi. Lakini alionyesha tabia ya kutoweza kudumisha ujumbe huo, wakati mmoja akihoji asili ya Harris na kuapa kuwalinda wanawake ” wapende au wasipende”.

Mbinu yake isiyodhibitiwa ilionekana kuwa iliyolenga kuwachochea wafuasi wake, badala ya kuongeza ushawishi wake.