Uhuru akumbana na ghadhabu za Wakenya jijini London
Na CHRIS WAMALWA akiwa jijini London, Uingereza
RAIS Uhuru Kenyatta mnamo Jumanne alikumbana na kundi la Wakenya wenye ghadhabu nje ya Jumba la Chatham, nchini Uingereza.
Punde baada ya kutoa hotuba yake katika jumba hilo, Wakenya hao wanaoishi mjini London walimkabili Rais Kenyatta kwa mabango na firimbi wakimshutumu kwa kukiuka haki za kibinadamu katika uongozi wake.
Iliwalazimu maafisa wa usalama kumkinga Rais na maafisa wake baada ya waandamaji hao kukaribia msafara wake wakiinua mabango yaliyokuwa yameandikwa ‘ Heshimu haki za kibinadamu’ na ‘heshimu uongozi wa sheria.’
Akiongea na Taifa Leo, mmoja wa waliopanga maandamano hayo, Bw Sebastian Onyango, alisema walitaka kuonyesha hasira zao kwa rais kwa kushindwa kuhakikisha haki imetendeka kwa zaidi ya Wakenya 350 waliopoteza maisha yao wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
“Tunaandamana kupinga ukiukaji wa haki za kibinadamu na kupuuzwa kwa maagizo ya korti na serikali ya (Rais) Kenyatta. Tunataka mageuzi ya uchaguzi, haki katika jamii na kujumuishwa kwa jamii zote katika uongozi wa serikali,” alisema Bw Onyango.
Bw Onyango alimshutumu Rais Kenyatta kwa ‘kudanganya’ mataifa ya nje kuhusu hali ya kidemokrasia nchini Kenya, akisema serikali yake imekandamiza uongozi wa kidemokrasia kwa kuwadhulumu wafuasi wa upinzani na kukiuka maagizo ya mahakama.
Kundi hilo la waandamanaji lilipuuzilia mbali muafaka kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga likisema hauna lengo la kuwaunganisha Wakenya.
Kunufaisha wachache
Waandamanaji hao walisema muafaka huo unalenga tu kunufaisha watu wachache badala ya kuangazia masaibu ya mamilioni ya Wakenya wanaohangaika kutokana na ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.
“Tunataka jenerali wa vuguvugu la NRM, Miguna Miguna arejeshwe nyumbani Kenya na kufidiwa mateso aliyoyapata mikononi mwa serikali ya Jubilee.
Haifai kuwakubalisha raia wa nje kuja Kenya na raia wazaliwa wa Kenya wanatimuliwa kinyume cha sheria,”alisema kwenye taarifa iliyotumwa katika vyombo vya habari na baadhi ya Wakenya wanaoishi nje.
Kundi hilo linaongozwa na Janet Suton, Jennifer Kiplagat, Kevin Were, Aggrey Kikaya, Maurice Owidi na Sebastian Onyango.
Mwaka uliopita, kundi lingine la Wakenya lilimkabili kinara wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga eneo hilo hilo baada ya kutoa hotuba yake.
Katika hotuba yake Jumanne, Rais Kenyatta alisema serikali yake inaendelea na juhudi za kuhakikisha Wakenya wanaoishi nje ya nchi wameshirika katika uchaguzi mkuu wa 2022.