Kimataifa

Ujumbe wa Iran kwa Trump: Ukija vizuri tutakupokea, ukija vibaya pia utatupata

Na MASHIRIKA November 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Iran, imesema kuwa itaendelea kulinda maslahi yake, na kufuata chochote kinachowiana na imani yake hata wakati huu rais mpya wa Amerika, Donald Trump, anaposubiri kuapishwa.

Kauli hiyo ilitolewa na msemaji wa serikali ya nchi hiyo, Fatemeh Mohajerani, alipoulizwa kama kuna uwezekano wa kuwepo kwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya utawala wa nchi yake na ule wa Trump.

Hata hivyo, alitahadharisha kuwa uamuzi wa mwisho wa mazungumzo kati ya nchi hizo mbili utategemea mwanasiasa mkuu Ayatollah Ali Khamenei na Baraza Kuu la Usalama la Kitaifa.

“Kwa sasa, kilicho muhimu kwetu ni vitendo wala si maneno, lakini tunapendekeza Trump aziangalie upya sera zake za zamani,” Mohajerani alisema.

Hata hivyo, hakuna ripoti zozote kwamba Trump au timu yake wanapanga aina yoyote ya mazungumzo kati ya Amerika na Serikali ya Iran.

Rais huyo mteule alisema wakati wa kampeni yake kuwa, “Sitaki kuingilia Iran lakini nchi hiyo haiwezi kuwa na silaha za nyuklia.”

Trump aliiondoa Amerika katika mkataba wa nyuklia wa Iran wa mwaka 2015 na mataifa yenye nguvu zaidi duniani akiiongoza nchi hiyo mnamo 2018 na kuiwekea tena vikwazo ambavyo viliathiri vibaya uchumi wa Iran.

Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Washington na Tehran kuhusu kufufua mpango wa nyuklia yalianzishwa chini ya utawala wa Rais Joe Biden lakini yakakwama.

Naye Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, alisema Tehran haitaweza kupuuza adui yake mkuu, Amerika.

“Tupende au tusipende, tutalazimika kushirikiana na Amerika katika nyanja za kikanda na kimataifa, kwa hivyo ni bora kudhibiti uhusiano huu sisi wenyewe,” Rais Pezeshkian alisema.

Haya yanajiri huku Trump akiendelea kufanya uteuzi muhimu katika serikali yake. Rais huyo mteule natarajiwa kumteua Seneta wa Florida Marco Rubio kuwa waziri wa masuala ya kigeni na Mike Waltz kuwa mshauri wake wa masuala ya usalama wa taifa.

Waltz na Rubio wamekuwa na mitazamo hasi dhidi ya Iran China, ambayo wanaichukulia kama tishio na changamoto kwa nguvu zao kijeshi na kiuchumi.

Mnamo Jumatatu, Trump alimteua Elise Stefaniki ambaye ni mbunge wa Republican kutoka New York kuwa Balozi wa Umoja wa Kitaifa (UN).

Pia alimteua Tom Homan ambaye alikuwa mkurugenzi kwenye idara ya uhamiaji kuwa mmoja wa washauri wakuu katika awamu ya pili ya utawala wake na mkuu wa uhamiaji na mipaka, akimtwika jukumu la kutimiza ahadi yake ya kuwatimua wahamiaji wasio na vibali.

Wakati uo huo, Wakuu wa Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF, wamesema wako tayari kushirikiana na Trump. Wakuu hao aidha, wamesisitiza umuhimu wa kuzifadhili sekta binafsi kwenye nchi zilizoathirika na mabadiliko ya tabianchi.

Mkuu wa Benki ya Dunia, Kristalina Georgieva, aliliambia jopo la watalaamu kwenye mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP29 unaofanyika nchini Azerbaijan kwamba benki hiyo ilishawahi kufanya kazi na Trump hapo awali na kwamba wataendelea kushirikiana naye atakapoapishwa kuwa rais Januari 2025.

Georgieva amesema pia kwamba ana imani kubwa sekta ya binafsi za Amerika zitaendelea kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ili kuendeleza juhudi zilizoanzishwa hapo awali.