Upinzani nchini Tanzania walia ‘tabu zile zile’ za kukandamizwa na CCM uchaguzini
UPINZANI nchini Tanzania hautarajii uchaguzi ujao wa mabaraza ya miji kuwa wa haki ukidai dosari zilizoshuhudiwa katika maandalizi zinalenga kufaidi chama tawala cha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu alisema upinzani hauna matumaini ya kushinda viti katika uchaguzi huo baada ya wagombeaji wao wengi kuzimwa kuwania katika uchaguzi huo wa Novemba 27.
Ijumaa Novemba 15 ndio ilikuwa siku ya mwisho ya kupigwa msasa kwa wagombeaji, kulingana na ratiba iliyowekwa na Wizara ya Utawala wa Kikanda na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Mnamo Alhamisi, Waziri wa Tamisemi Mohamed Mchengerwa alisema kesi za rufaa dhidi ya kukataliwa kwa maombi ya wagombea kadhaa zitaangaliwa upya kabla ya orodha ya mwisho ya wagombeaji kutayarishwa.
Lakini siku iliyofuata, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Emmanuel Nchimbi aliitaka Wizara hiyo “kupuuzilia mbali” makosa madogo yaliyofanywa na wagombeaji wakati wa kujaza fomu zao “ili Watanzania zaidi wawe na nafasi ya kuwania viti katika uchaguzi.”
Bw Nchimbi alisema ushauri wake ulikuwa na “baraka” za Rais Samia Suluhu, mwenyekiti wa chama hicho.
Zaidi ya viti 80,000 vya wenyeviti na 480,000 vya wanachama wa mabaraza vinashindaniwa katika ngazi za kijiji, barabara na vitongoji.
Wizara ya Tamisemi inayosimamiwa na Afisi ya Rais, imepewa wajibu wa kusimamia chaguzi hizo.
Wajibu wa wizara hiyo katika uchaguzi huo, hata hivyo, umepingwa kwani mageuzi ya sheria yaliyotekelewa juzi yaliitwika tume ya uchaguzi wajibu wa kusimamia chaguzi za mabaraza ya miji.
Baadaye mahakama iliamua kuwa sheria inafaa kufafanuliwa kwa namna itakayohakikisha kuwa chaguzi za mabaraza ya miji pia zinaendeshwa na tume ya uchaguzi, itakayoendesha chaguzi za urais na ubunge mwaka ujao.
Vyama vya upinznai vikiongozwa na Chadema na ACT Wazalendo vimelalamika vikali kwamba maelfu ya wagombeaji wao wameondolewa kutoka orodha ya wagombeaji bila sababu maalum, na maafisa tangu ukaguzi wa wagombeaji ulipoanza Novemba 8.
Haya yalijiri baada ya shughuli ya usajili wa wapiga kura iliyokumbwa na utata. Hii ni baada ya Wizara ya Tamisemi kushutumiwa kujaza sajili ya wapiga kura na watu wasiohitimu kama vile wanafunzi waliofikisha umri wa kupiga kura na watu waliokufa ili kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura.
Wadadisi wa kisiasa wamebaini usawa kati ya namna maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mtaa mwaka huu yanavyofanywa na uchaguzi wa udiwani wa mwaka wa 2019.
Uchaguzi huo ulitoa nafasi ya kuendeshwa kwa uchaguzi mkuu wa 2022 uliokumbwa na utata na ambapo CCM ilipata ushindi mkubwa huku upinzani ukilemewa kabisa.
Kulingana na matokeo rasmi kutoka kwa uchaguzi huo wa 2019, chama cha CCM kilishinda asilimia 99.9 ya viti katika ngazi za vijiji, asilimia 100 ya viti katika ngazi za barabara na asilimia 99.4 ya viti katika ngazi za vitongoji.
Akiongea na wanahabari katika mji wa Singida Ijumaa, Bw Lissu alisema Chadema haina matumaini katika chaguzi hizo kwa sababu maandalizi yake yamevurugwa.
“Shughuli zote zimevurugwa kuanzia usajili wa wapiga kura na usajili na kuchujwa kwa wagombea. Upinzani sasa unafaa kujipanga upya kuanza mchakato mpya wa kupigania mageuzi ya kidemokrasia,” akasema.
“Kwa mfano, tayari takwimu zinaonyesha kuwa angalau wagombeaji 100,000 wa Chadema wamezuiwa kuwania viti kutokana na sababu finyu ilivyokuwa wakati ulipita. Na hatuna muda wa kutosha kukata rufaa dhidi ya hatua hiyo ili waruhusiwe kuwania,” Bw Lissu akasema.
Alisema Wizara ya Tamisemi imehakikisha kuwa uchaguzi huo umekamilishwa hata kabla ya kura ya kwanza kupigwa.
Bw Lissu alisema kuwa katika Dar es Salam pekee zaidi ya asilimia 95 ya wagombeaji wa Chadema wa viti vya viwango vya vijiji, barabara na vitongoji wamezuiwa kuwania.
Nacho chama cha ACT-Wazalendo kilisema kwenye taarifa kuwa zaidi ya wagombeaji wake 50,000 (asilimia 60) wamezimwa kuwania.
Malalamishi sawa na hayo yalitoka kwa vyama vya Civic United Front na NCCR-Mageuzi.