• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Upinzani Sudan wakataa mazungumzo na wanajeshi

Upinzani Sudan wakataa mazungumzo na wanajeshi

Na AFP

VIONGOZI wa upinzani nchini Sudan wamekataa kushiriki mazungumzo na Baraza Tawala la Kijeshi (TMC) na kuitisha haki kufuatia operesheni inayoendelezwa dhidi ya waandamanaji ambayo imesababisha vifo vya watu 108 kufikia Jumatano.

“Wananchi wa Sudan hawako tayari wa mazungumzo,” akasema Amjad Farid, msemaji wa Chama cha Wataalamu Nchini Sudan (SPA).

Chama hicho ndicho kiliongoza maandamano yaliyosababisha kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar al- Bashir.

“Hatuko tayari kuongea na Baraza Tawala la Kijeshi (TMC) ambalo linawaua wananchi. Tunataka haki na uwajibikaji kwanza kabla ya kushiriki mazungumzo yoyote kuhusu mchakato wowote wa kisiasa,” akaambia shirika la habari la AFP.

Vikosi vya usalama viliwashambulia waandamanaji ambao wamekuwa wakipiga kambi nje ya makao makuu ya kijeshi jijini Khartoum.

Inasemekana kuwa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF), ambacho makundi ya kutetea haki za kibinadamu yanadai kiliundwa kutokana na kundi la wapiganaji la Janjaweed, ndilo lilihusika na mashambulio hayo. Kundi la Janjaweed linahusishwa na mauaji ya halaiki katika eneo la Darfur yaliyodumu kwa miaka 16.

Kamati ya Muungano wa Madaktari Nchini Sudan inayounga mkono waandamanaji ilisema kufikia Jumatano jumla ya watu 108 walikuwa wameuawa katika operesheni hiyo huku wengine 500 wakijeruhiwa. Idadi hiyo inajumuisha miili ya watu 40 ilipatikana katika mto Nile.S

Sudan imekuwa chini ya uongozi wa baraza la kijeshi tangu kuondolewa mamlakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar al- Bashir mnamo Machi mwaka huu kutokana na maandamano ya raia waliopinga utawala wake wa kiimla. Wanajeshi hao waliahidi kuongoza kwa miaka mitatu kabla ya kupisha utawala.

Lakini Kiongozi wa Kijeshi Abdel Fattah al-Burha alisema makubaliano hayo sasa yamewekwa kando na kwamba uchaguzi utafanyika ndani ya kipindi cha miezi tisa- mpango ambao ulikataliwa na waandamanaji.

Na mnamo Jumatano, Burhan alisema kuwa wako tayari kwa mazungumzo kuhusu mzozo nchini Sudan bila masharti yoyote, pendekezo ambalo kwa mara nyingine lilikataliwa na waandamanaji.? Farid alisema chama chake cha SPA na vuguvugu la Alliance for Freedom and Change wataendelea kutumia mbinu zozote zisizo za fujo na maasi kupinga utawala wa TMC.

Hatua ya upinzani kukataa mazungumzo kunajiri baada la kamanda wa kikosi cha RSP aliyeshutumiwa kutekeleza mauaji ya raia alisisitiza kuwa taifa hilo halitaruhusiwa kutumbukia katika fujo.

“Hatutaruhusu fujo… sharti tuhalinde ukuu wa taifa kupitia sheria,” Mohamed Hamdan Dagalo, naibu kiongozi wa baraza la kijeshi, waliwaambia wanajeshi wake kwenye hutoba kupitia runinga.

You can share this post!

Kalonzo hafai urais 2022, Musila ashikilia

Mamapima awatuza walevi sugu unga na mafuta

adminleo