Kimataifa

Upinzani Tanzania wadai Lissu hapatikani gerezani alikozuiliwa

Na REUTERS April 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, kilisema Ijumaa kwamba hakijui aliko kiongozi wake Tundu Lissu, baada ya kuhamishwa kutoka gereza alilokuwa akizuiliwa kufuatia kukamatwa kwake wiki iliyopita kwa tuhuma za uhaini.

Viongozi wa CHADEMA, mawakili wa Lissu na jamaa zake walisema walijaribu mara kadhaa kumtembelea katika gereza la Keko jijini Dar es Salaam, ambako amekuwa akizuiliwa tangu Aprili 9  bila mafanikio.

“CHADEMA kinaitaka Idara ya Magereza pamoja na taasisi husika za serikali kutoa taarifa kuhusu alikopelekwa Lissu,” chama hicho kilisema katika taarifa.

Hata hivyo, Idara ya Magereza ilikanusha kuwa Lissu amehamishwa kutoka gerezani.

“Taarifa hiyo si ya kweli. Tunapenda kuufahamisha umma kuwa Tundu Lissu yuko salama na bado anazuiliwa katika Gereza la Keko jijini Dar es Salaam kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi,” alisema msemaji wa Idara ya Magereza, Elizabeth Mbezi.

Lissu, aliyeibuka katika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2020, alishtakiwa kwa kosa la uhaini wiki iliyopita kutokana na kile ambacho waendesha mashtaka walisema ni hotuba aliyotoa akirai wananchi kuzua uasi na kuvuruga uchaguzi. Hajaruhusiwa kujibu mashtaka hayo mahakamani.

Mashtaka haya yameibua upya mjadala kuhusu rekodi ya haki za binadamu ya Rais Samia Suluhu Hassan anapojitayarisha kugombea urais mwaka huu.

Wikiendi iliyopita, Tume ya Uchaguzi ilitangaza kuwa CHADEMA kitazuiwa kushiriki uchaguzi wa Oktoba kwa kukataa kutia saini mkataba wa maadili ya uchaguzi kikishinikiza marekebisho ya mfumo wa uchaguzi.

Baada ya kuchukua uongozi mwaka 2021,Rais Suluhu alipongezwa kwa kulegeza ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa na uthibiti mkali wa vyombo vya habari wakati wa utawala wa mtangulizi wake, John Magufuli, aliyefariki akiwa madarakani.

Hata hivyo, amekosolewa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu kutokana na msururu wa visa vya kukamatwa kwa wapinzani wa kisiasa, kutoweka kwa watu kiholela na mauaji ya kutatanisha.

Rais Hassan amesema serikali yake imejikita katika kuheshimu haki za binadamu, na mwaka jana aliagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu visa vya watu kutekwa.