Kimataifa

Ushindi wa Democrats wamweka Netanyahu matatani

Na REUTERS November 5th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

JERUSALEM, Israel:

WAPINZANI wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wametumia ushindi wa chama cha Democrats katika uchaguzi wa katikati ya muhula Amerika kumshutumu kwa kuharibu uhusiano wa muda mrefu wa Israel na vyama vikuu vya kisiasa Amerika.

Democrats walipata viti vingi katika Seneti na Bunge la Congres katika uchaguzi wa Jumanne, Novemba 3, matokeo ambayo ni pigo kwa Rais Donald Trump, huku hasira za wapigakura kuhusu vita vya Amerika na Israel dhidi ya Iran zikichangia matokeo hayo.

Ushindi huo unajiri wiki moja baada ya muungano wa mrengo wa Netanyahu kupoteza wingi wa viti katika uchaguzi wa Israel.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Democrats nchini Israel, Yair Golan, alisema matokeo hayo yanaonyesha jinsi Netanyahu alivyopoteza uungwaji mkono Amerika.

“Matokeo yanaonyesha jinsi Netanyahu alivyo sumu kisiasa miongoni mwa Democrats na Republican,” akasema.

Kiongozi mwengine wa upinzani, Yair Lapid, alisema Israel haiwezi kumudu kuendelea kuwa na Netanyahu mamlakani.

“Anahatarisha usalama wetu, anadhoofisha demokrasia yetu na ataharibu hadhi yetu katika kiwango cha kimataifa,” akasema.

Amerika imekuwa mshirika mkuu wa Israel kwa miongo kadhaa, ikitoa mabilioni ya dola kama msaada wa kijeshi tangu miaka ya 1970.

Hata hivyo, uungwaji mkono huo umepungua kutokana na vita Gaza na mashambulizi dhidi ya Iran.

Trump, ambaye alikuwa amemuunga mkono Netanyahu, aliahidi kusitisha msaada wa kila mwaka wa dola bilioni nne kwa Israel.

Profesa Udi Sommer wa Chuo Kikuu cha Tel Aviv alisema Bunge jipya linalotawaliwa na Democrats linaweza kuiwekea Israel shinikizo kupitia uchunguzi na maamuzi ya bajeti.

“Ushindi mkubwa wa Democrats na kushindwa kwa Republican vinaashiria sura mpya ya uhusiano kati ya Amerika na Israel,” akasema.

Rais Isaac Herzog anatarajiwa kuanza mashauriano kuhusu kuunda serikali mpya wiki hii.