Mabadiliko katika uume yanayohitaji ushauri wa daktari haraka upesi
MABADILIKO katika uume yanaweza kuwa ishara ya matatizo makubwa ya kiafya, yakiwemo kisukari, magonjwa ya figo na saratani, hii ni kulingana na utafiti ulioangazia dalili ambazo wanaume wengi hupuuza.
Mtaalamu wa Masuala ya Matibabu, Shafi Wardak, wa kliniki ya The Forbury, Uingereza, kwenye utafiti huo, anaonya kuwa wanaume hawapaswi kumakinik ia uwezo wa uume kupata ashiki pekee, bali pia mabadiliko mengine yasiyo ya kawaida katika kiungo hicho.
Kati ya dalili ambazo zinaonyesha huenda mambo si kawaida, ni mabadiliko ya kukojoa. Kukojoa mara nyingi kunaweza kuashiria kisukari, maambukizi kwenye njia ya mkojo au kuongezeka kwa tezi dume.
Mkojo dhaifu unaweza kuashiria kuziba kwa njia ya mkojo au saratani ya tezi dume. Kukojoa kidogo na mkojo mweusi kunaweza kuashiria upungufu wa maji mwilini au matatizo ya figo.
Pia kuna vipele na vidonda kwenye uume ambavyo vinaweza kusababishwa na magonjwa ya zinaa au saratani ya uume. Vidonda visivyouma vinaweza kuwa ishara ya maradhi kama kaswende.
Mabadiliko ya ngozi pia ni ya kuangaliwa kwa kuwa kubadilika rangi, kuchubuka kunaweza kuashiria magonjwa ya ngozi au maambukizi yanayohitaji uchunguzi wa kina wa daktari.
Uume kupinda wakati wa ashiki na kusababisha maumivu kunaweza kuashiria ugonjwa wa ‘Peyronie’, unaosababishwa na kovu kujijenga ndani ya misuli za uume.
Pia harufu na mabadiliko ya shahawa ni jambo la kutathminiwa.
Harufu isiyo ya kawaida inaweza kuashiria uvimbe wa kichwa cha uume nako kupungua kwa shahawa au nguvu ya kumwaga kunaweza kuhusishwa na kisukari, upungufu wa homoni za kiume au kuzibwa kwa mirija.
Wardak anashauri wanaume kuosha sehemu za siri kwa maji na sabuni isiyo kali na kuvaa chupi safi zinazopitisha hewa.
“Hata mabadiliko madogo katika, rangi au mwonekano wa ngozi, kama vile vipele, uvimbe au madoadoa, yanapaswa kuzingatiwa. Ingawa baadhi ya mabadiliko yanaweza kusababishwa na mwasho mdogo, mengine yanaweza kuashiria maambukizi au magonjwa yanayoandama sehemu za siri,” akasema Wardak.
Wataalamu wanasisitiza kuwa dalili hizi hazithibitishi moja kwa moja ugonjwa fulani, hivyo ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu badala ya kujitibu.