Kimataifa

Wabunge 16 wa Tanzania wahusika kwenye ajali wakielekea michezoni Mombasa

Na  THE CITIZEN December 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WABUNGE 16 kutoka Tanzania walijeruhiwa ajalini wakisafiri kuelekea Mombasa kushiriki michezo ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ajali hiyo ilitokea basi walimokuwa wakisafiria lilipogongana na lori mapema Ijumaa.

Pia, maafisa wawili wa bunge na dereva wa basi hilo linalomilikiwa na Kampuni ya Shabiby walijeruhiwa kwenye ajali hiyo, iliyotokea katika eneo la Mbande, Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (RPC), Bw George Katabazi, alisema ajali hiyo ilitokea saa nane usiku.

Alisema basi hilo liligongana na lori lililokuwa likitoka Morogoro kuelekea Dodoma.

“Chanzo cha ajali ni kwamba dereva wa basi la Shabiby lililokuwa limebeba wabunge na maafisa wa bunge hakuchukua tahadhari alipokuwa akipita gari lingine, na kusababisha basi kugongana na lori,” alisema Bw Katabazi.

Kulingana na kamanda huyo, dereva wa basi hilo alikamatwa kwa kusababisha ajali hiyo.

“Waathiriwa hao wanapokea matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, na Hospitali ya Uhuru,” alisema kamanda huyo wa polisi wa mkoa.

“Wito wangu ni kwa kila mtu kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali, ambazo mara nyingi husababisha vifo, majeraha, na uharibifu mkubwa wa mali. Madereva wanapaswa kuepuka uzembe na mwendo wa kiholela,” alisisitiza.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA