Kimataifa

Wakamatwa kwa kushukiwa walipanga kuroga rais

Na MASHIRIKA December 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WANAUME wawili wamekamatwa nchini Zambia wakituhumiwa kuwa “waganga” waliokuwa wametwikwa jukumu la kujaribu kumroga rais.

Kulingana na vyombo vya habari vya  Zambia, polisi walisema waliwakamata Jasten Mabulesse Candunde na Leonard Phiri katika mji mkuu, Lusaka.

“Lengo lao lilidaiwa kuwa kutumia hirizi kudhuru” Rais Hakainde Hichilema, ilisema taarifa ya polisi, iliyotolewa Ijumaa.

Watu wengi katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika wanaamini – na wanaishi kwa hofu ya – uchawi.

Polisi walisema Bw Candunde na Bw Phiri waliajiriwa na Nelson Banda, nduguye mdogo wa Mbunge Emmanuel “Jay Jay” Banda.

Mbunge huyo aliripotiwa kukamatwa mwezi uliopita katika nchi jirani ya Zimbabwe kutokana na mashtaka ya wizi, ambayo anayakanusha, lakini hajaonekana hadharani.

Pia anadaiwa kutoroka kutoka kizuizini mwezi Agosti alipokuwa akisubiri kufikishwa mahakamani.

Chama cha upinzani cha Patriotic Front (PF), kinachoongozwa na Rais wa zamani Edgar Lungu, hapo awali kilidai kuwa mashtaka hayo yanachochewa kisiasa.

Emmanuel Banda, ambaye amekuwa mbunge huru tangu 2021, awali alihusishwa na Lungu, ambaye alipoteza urais kwa Hichilema katika uchaguzi mwaka huo.

Katika taarifa yao, polisi walisema kwamba kaka mdogo wa mbunge huyo, Nelson, “kwa sasa yuko mafichoni”.

Bw Candunde na Bw Phiri wameshtakiwa chini ya Sheria ya Uchawi ya Zambia kwa “kumiliki hirizi”, “kudai wana ujuzi wa uchawi” na “ukatili kwa wanyama pori”.

Wawili hao walipatikana na “hirizi mbalimbali”, akiwemo kinyonga aliye hai, polisi waliongeza.

Waliwaambia polisi walikuwa wameahidiwa mamilioni ya pesa wakifaulu katika  kazi yao, kulingana na taarifa ya polisi.

Washukiwa hao wanazuiliwa na watafikishwa mahakamani “hivi karibuni”, polisi walisema, lakini hawakutoa tarehe kamili ya kusikilizwa kwa kesi hiyo. Bado hawajazungumza hadharani kuhusu tuhuma hizo.