Kimataifa

Wakili aliyemshtaki Trump ajiuzulu siku 7 kabla ya serikali mpya kuingia mamlakani

Na MASHIRIKA January 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WASHINGTON D.C. AMERIKA

WAKILI maalum aliyeongoza kesi mbili dhidi ya Donald Trump amejiondoa katika Idara ya Haki nchini Amerika kabla ya rais huyo mteule aliyewania kwa chama cha Republican kutawazwa rasmi kwa hatamu ya pili Januari 20.

Jack Smith aliongoza kesi mbili zilizomhusisha Trump na madai ya kutumia vibaya nakala zinazosheheni siri za nchi baada ya kuondoka ikulu ya White House na kujaribu kupindua matokeo aliposhindwa katika uchaguzi wa urais mnamo 2020.

“Wakili maalum alikamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti yake ya mwisho ya siri Janauari 7, 2025, na kujitenga na idara hiyo Januari 10,” walisema maafisa katika nakala iliyowasilishwa kwa Jaji Aileen Cannon.

Walimsihi Jaji asiongeze muda wa amri aliyotoa ya kuzuia ripoti ya mwisho ya Smith kutolewa.

Smith aliyekuwa mwendeshaji mashtaka kuhusu maovu ya kivita, aliteuliwa 2022, karibu miaka miwili baada ya shambulizi kwenye majengo ya bunge, Capitol, Amerika, kuongoza Idara ya Haki katika uchunguzi uliokuwa ukiendelea dhidi ya Trump.

Aliwasilisha kesi mbili miongoni mwa nne zilizomkabili Trump baada ya kuondoka afisini lakini akakwama wakati jaji wa Florida aliyeteuliwa na Trump kutupilia mbali kesi moja nayo mahakama ya kilele Amerika ikibaini kuwa marais wa zamani wamekingwa kutokana na kushtakiwa kuhusiana na vitendo vya afisi.

Kesi zote mbili hazikuwasilishwa katika kikao rasmi kortini.

Baada ya Trump kumbwaga naibu rais wa Democratic, Kamala Harris katika uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba 5, Smith alitupilia mbali kesi zote mbili akitaja sheria ya muda mrefu katika idara ya haki inayowakinga marais wanaohudumu kushtakiwa.

Trump ambaye mara kwa mara amemwita Smith “mwendawazimu” na kusema atampiga kalamu pindi tu akakapochukua afisi, amedokeza huenda akamwadhibu Smith na wengine waliomchunguza arejeapo mamlakani.