Kimataifa

Wanaharakati 36 wakamatwa DRC kupinga ada za simu

September 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA MASHIRIKA

WANAHARAKATI 36 Jumapili walikamatwa nchini humu kwa kuongoza maandamano ya kupinga ada za juu za mawasiliano zinazotozwa na kampuni ya Airtel.

Watu hao ambao ni wanachama wa kundi la kutetea utawala wa kidemokrasi, maarufu kama Lucha Movement, pia walidaiwa kutoa matamshi ya kuwaharibia sifa wasimamizi wa kampuni hiyo ya mawasiliano kutoka India.

Maandamano hayo yalifanyika katika mji wa Goma, mashariki mwa DRC, msemaji wa vuguvugu hilo Steward Muhindo aliambia AFP.

Wanachama wa kundi hilo wanaitaka Airtel kupunguza bei ya kupiga simu katika miji yote ya taifa hilo linalozongwa na umaskini, na watu wanapokea mapato ya Dola mbili (Sh200) kwa siku.

Waandamanaji 13 walifungiwa katika gereza la Central jijini Goma.

“Na wengine 23 walipelekwa kwa afisi ya mwendesha mashtaka mkuu,” Bw Muhindo akasema.

Na kufuatia kukamatwa kwo, jumla ya mashirika 36 ya kutetea haki nchini DRC yaliikashifu serikali ya Rais Felix Tshisekedi.