Wanaobusu maiti TZ waonywa watajiambukiza Ebola
MASHIRIKA Na PETER MBURU
SERIKALI ya Tanzania imetoa tahadhari kwa wananchi wake kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi ya kidemokrasia ya Congo (DRC), ikitahadharisha zaidi watu wanaoendeleza desturi za kubusu maiti kuwa wamo hatarini.
Kupitia ujumbe uliotolewa na wizara ya ya afya ya taifa hilo, mlipuko wa ugonjwa huo hatari katika nchi ya DRC ni sababu ya kuwajalisha, na sasa serikali inataka kuwaelimisha wananchi kuhusu njia zote za kujikinga.
“Sasa sisi kama serikali na kama Wizara ya Afya tuna wajibu wa kutoa elimu kwa wananchi wetu na kwa umma wa Tanzania ili waweze kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola. Mojawapo ya njia za kujikinga kupokea ugonjwa huu ni kuepuka kugusa damu au majimaji ya mtu ambaye tayari amepokea ugonjwa huu,” akasema Dkt Leonad Subi, mkurugenzi wa huduma za kinga wizara ya afya nchi hiyo.
Dkt Subi aidha alieleza kuwa kunao wanyama wanaobeba virusi vya ugonjwa huo, na ambao Watanzania Fulani huwala.
“Hata kunao wanaopenda kula wanyamapori kama sokwe ambao pia wanaweza wakawa wamebeba virusi vya ugonjwa wa Ebola.”
Na tahadhari ya kipekee ilitolewa kwa watu wanafanya mila na desturi zinazokusana na maiti kuwa makini zaidi wakati huu.
“Ni vizuri tukaepuka mila na desturi ambazo zaweza zikachangia maambukizi ya ugonjwa wa ebola. Kwa mfano kunao wanaopenda kubusu maiti, kuna wengine wanapenda kukumbatia haswa wakati wa mazishi na mengineyo,” akasema Dkt Subi.
Alizidi kusema kuwa taifa hilo linalenga kushirikiana na mataifa jirani kama kenya, Burundi na Uganda kwa ajili ya kuwalinda wananchi wake waliosafiri katika mataifa hayo.