Wasanii Wakristo waliokataa kutengeneza kadi za mialiko ya harusi za mashoga wapata haki
Na AFP
WASHINGTON D.C., Amerika
JUMUIYA ya mashoga na wasagaji Amerika imepata pigo kuu baada ya Mahakama ya Kilele kuamua kwamba wasanii wawili wa Arizona waliokataa kutengeneza kadi za mialiko kwa harusi za jinsia moja kutokana na imani yao ya Kikristo walikuwa na haki kufanya hivyo.
Mahakama hiyo ilifutilia mbali hukumu za awali dhidi ya wanawake wawili hao za kukiuka “sheria kuhusu mahusiano ya binadamu” zilizoanzishwa na mji wa Kusini Magharibi wa Phoenix kulinda haki za mashoga na wasagaji.
Wasanii hao wangekabiliwa na kifungo cha hadi miezi sita gerezani na faini ya Sh259,223 kila wakati ambapo wangekataa kutengeneza mialiko kwa harusi za mashoga.
Joanna Duka na Breanna Koski, wamiliki wa kampuni ndogo ya sanaa ya uchoraji inayojihusisha na mialiko iliyoandikwa, walishtaki mji huo 2016 kuhusu sheria hiyo.
Hawakuwa wamepatiwa kazi na ‘wanandoa’ wowote wa LGBTQ.
Wawili hao walijitetea kwa kusema kwamba imani yao ya Kikristo inawazuia kupigia chapuo ndoa kati ya watu wa jinsia moja, ikiwemo kutengeneza kadi za mwaliko.
Isitoshe, walisema kuwa, sheria ya Phoenix ingewashurutisha kukiuka haki yao ya kujieleza na dini.
“Imani ya Duka na Koski kuhusu ndoa jinsia moja inaweza kuonekana kama iliyopitwa na wakati au ya kuchukiza kwa baadhi ya watu,” korti ilisema katika uamuzi wake.
“Lakini haki za uhuru wa kujieleza na haki za dini si kwa wale tu wanaoonekana kuwa na ufahamu, kuendelea au walio juu. Ni za kila mtu,”
Japo majaji hao hawakupanua uamuzi huo kushughulikia shughuli zote za kibiashara, watetezi wa haki za mashoga walionya kwamba uamuzi huo umeandaa jukwaa kwa makabiliano zaidi kisheria.
“Uamuzi huu umefungua mlango kwa wamiliki wengine wenye mtazamo finyu kubagua wazi watu wa LGBTQ kuhusu jinsi tulivyo na tunayempenda,” alisema Brianna Westbrook, naibu mwenyekiti wa chama cha Arizona Democratic Party, ambaye ni mwenye utata kijinsia.
“Mmiliki wa biashara sasa ataweza kuchapisha kwenye tovuti yake au kuweka ishara kwenye lango lake akisema ‘watu wasio mashoga au wasagaji pekee,” alionya Westbrook.
Walalamishi hao waliwakilishwa na Alliance Defending Freedom (ADF), shirika la wanajadi ambalo limejitolea kukabiliana na sheria sawa na hizo kote Amerika.
Habari hii imetafsiriwa na MARY WANGARI