Wasiwasi wa Ruto kuhusu mzozo wa mashariki mwa DRC
HALI inayoendelea kudorora katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inazua wasiwasi kwa nchi jirani, Rais William Ruto amesema.
Akihutubia mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), ambao aliongoza kwa pamoja na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa Rais Ruto alisema kuwa vita vinavyoendelea katika DRC vinaweza kusambaa na kuleta madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na vifo, msukosuko, na kuwafanya maelfu ya watu kuwa wakimbizi.
Wakati huo huo, mkutano huo ulipitisha utekelezaji wa hatua za haraka, za muda wa kati, na za muda mrefu ili kufanikisha amani na usalama wa kudumu Mashariki mwa DRC.
Katika kikao hicho, marais wa zamani Uhuru Kenyatta (Kenya), Olusegun Obasanjo (Nigeria), na Kgalema Motlanthe (Afrika Kusini) waliteuliwa kuwa sehemu ya jopo la kutafuta amani katika eneo hilo.
Pia, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Catherine Samba, pamoja na Rais wa zamani wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde, waliteuliwa kwenye jopo hilo.
DRC inakabiliwa na mojawapo ya migogoro mikubwa ya wakimbizi na kibinadamu ulimwenguni, hali inayolazimu mamilioni ya watu kuhama makazi yao.
Mnamo Januari, waasi wa kundi la M23 waliteka na kutwaa Goma, mji mkuu wa jimbo lenye utajiri wa madini la Kivu Kaskazini, na mwezi Februari, waliteka Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini.
Waasi hao wameendelea kusonga kuelekea Magharibi, hali inayozua hofu zaidi katika eneo hilo.