Kimataifa

Watu 48 wafa katika ajali ya trela ya mafuta na lori lililobeba watu na ng’ombe, Nigeria

September 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WATU 48 wameuawa katika jimbo la Niger, Nigeria baada ya trela moja la kusafirisha mafuta kugongana na lori moja lililokuwa limebeba watu na ng’ombe, shirika la kupambana na majanga nchini humo limesema.

Shirika la Kupambana na Majanga katika Jimbo la Niger (NSEMA) lilisema ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa saba na dakika 30 usiku Jumapili.

Moto mkubwa ulitokea pindi magari hayo mawili yalipogongana

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la NSEMA Abdullahi Babaarah alisema maafisa wake walitumwa eneo la mkasa kuendesha shughuli za uokoaji.

Video ya eneo la tukio muda mfupi baada ya ajali hiyo inaonyesha magari hayo mawili yakiwa yameteketea kabisa pamoja na ng’ombe kadhaa.

Mhudumu moja wa shirika la NSEMA aliambia shirika la habari la Reuters kwamba waliokuwa wanajizatiti kutoa miili ya wafu kutoka kwa mabari ya magari hayo na mizoga ya wanyama hao.

Duru katika utawala wa jimbo hilo zilisema kuwa miili hiyo itazikwa katika makaburi ya pamoja.

Gavana wa Jimbo la Niger Umaru Bago, kwenye rambirambi zake kwa familia za waathiriwa alisema “nimezongwa na machungu kutokana na ajali hiyo.”

Visa vya kulipuka kwa matrela ya kusafirisha mafuta na ajali za kila mara zimekithiri zaidi Nigeria, kutokana na ubovu wa barabara.