Watu 500 wameuawa katika mashambulio nchini Syria – UN
Na AFP
UMOJA WA MATAIFA
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amesema kwamba watu 500 wakiwemo watoto 120, wameuawa katika muda wa wiki moja katika mashambulio ya ndege mashariki ya Ghouta nchini Syria na kutaja hali hiyo kama jehanamu ulimwenguni.
Bw Guterres alisema hayo wakati ambao Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, likiungwa na Urusi, lilipitisha kwa kauli moja amri ya kusitishwa kwa vita nchini Syria kwa siku 30 kuruhusu misaada ya kibinadamu na dawa kufikia waathiriwa.
Azimio la kusitisha mapigano hayo mara moja lilipitishwa wakati wanajeshi wa serikali ya Syria walipokuwa wakiendelea kuponda ngome za waasi eneo la Mashariki ya Ghouta, ambapo mamia ya watu wameuawa katika mashambulio ya wiki moja.
“Tumechelewa kukabiliana na mzozo huu, tumechelewa sana,” Balozi wa Amerika aliambia baraza baada ya kura na kulaumu Urusi kwa kuwa kikwazo kwa kura hiyo.
Azimio hilo linataka kusitishwa kwa vita mara moja kote Syria ili kuruhusu misaada kuwafikia wagonjwa na waliojeruhiwa bila kutatizwa.
Ili Urusi iweze kuunga mkono azimio hilo, ilibidi lugha iliyotumiwa ibadilishwe kufafanua kuwa lingetekelezwa bila kuchelewa badala ya kuwa lingeanza kutekelezwa saa 72 baada ya kupitishwa.
Mabalozi walisema walikuwa na hakika kwamba hatua hii isingefungua milango ya kuahirisha kusitishwa kwa vita, kwa sababu wanachama wa baraza walikuwa wameweka wazi kwenye majadiliano kwamba amri ingetekelezwa haraka.
Mabalozi hao walisema kwamba Guterres ataarifu baraza kuhusu hali ya utekelezaji wa azimio hilo katika muda wa siku 15.
Inasemekana Russia ilikubali kuunga azimio hilo baada ya kuthibitishiwa kuwa halitaathiri mashambulio dhidi ya kundi la kigaidi la Islamic State au Al-Qaeda, pamoja na watu, makundi na mashirika yanayohusishwa na vitendo vya kigaidi.
Hatua hii itaruhusu serikali ya Syria kuendelea kushambulia magaidi wanaoshirikiana na Al-Qaeda eneo la Idlib, mkoa wa mwisho unaodhibitiwa na magaidi nchini Syria.
Kulingana na azimio hilo, mashambulio yatakomeshwa maeneo ya Ghouta Mashariki, Yarmouk, Foua na Kefraya.