Kimataifa

Watu milioni 2 hatarini kufa njaa Zimbabwe

August 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

ZAIDI ya watu milioni mbili nchini Zimbabwe wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na kiangazi kilichoathiri mimea ya chakula na kuchangia mavuno duni, Shirika la Chakula Duniani (WFP) limesema katika ripoti yake ya hivi punde.

Kufuatia hali hiyo, shirika hilo limeanzisha mchango wa dola 331 milioni za Amerika (Sh33.2 bilioni) kwa ajili ya kuwasaidia waathiriwa katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.

“Kiangazi kama cha sasa hakijawahi kushuhudiwa nchini Zimbabwe kwa miaka mingi. Watu wataangamia kwa njaa ikiwa hawatapewa misaada ya kibinadamu kwa haraka,” Mkurugenzi Mkuu wa WFP, David Beasley alisema Jumatano, alipokuwa akianzisha mpango wa kutoa msaada jijini Harare Jumatano.

Inakisiwa kuwa takriban watu 5.5 milioni- thuluthi moja ya wananchi wa Zimbabwe- watahitaji misaada ya chakula kufikia 2020, kulingana na ripoti hiyo.

Baa la njaa nchini Zimbabwe ni matokeo ya kiangazi kilichoshuhudiwa nchini humo kuanzia Oktoba mwaka jana hadi Mei mwaka huu.

Hali hiyo pia inatokana na kimbunga kilichoshuhudiwa mashariki kwa nchini hiyo mwaka jana kilichoharibu mimea ya chakula, hasa katika maeneo ya mashambani.

WFP pia ilisema hali hiyo ya kiangazi imesababisha vianzo vya maji kukauka na mamilioni ya watu nchini Zimbabwe sasa hawawezi kupata maji safi.

Nchi hiyo pia inakabiliwa na changamoto za kudorora kwa uchumi, hali ambayo imeathiri pakubwa maisha ya wananchi kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha.

Roseline Marenyi, 30, mama wa watoto wawili anayeishi katika kitongoji cha Mbare jijini Harare aliwaambia wanahabari kwamba, amelazimika kupunguza kiwango cha chakula kwa familia yake kutokana na ongezeko la bei.

“Maisha ni magumu. Tunaweza kumudu chakula mara mbili tu kwa siku na hii inaweza kuathiri afya ya watoto. Tumezongwa na umasikini mwaka huu kuliko mwaka mwingine,” Bi Marenyi akaeleza.

Kutokana na kiangazi, wakazi wa vitongoji kadhaa jijini Harare na miji mingine ya karibu hupata maji safi kwa siku moja kwa wiki.