Watu wasiojulikana watuma barua yenye sumu kwa Trump
Na MASHIRIKA
NEW YORK, Amerika
MAAFISA wa usalama wamenasa kifurushi kilichotumwa kwa kiongozi wa Amerika Rais Donald Trump.
Kulingana na maafisa wa usalama, kifurushi hicho kilichokuwa na barua kilinaswa kabla ya kufikishwa katika Ikulu ya White House.
Barua hiyo yenye sumu iligunduliwa na maafisa wa usalama waliokuwa wakikagua vifurushi vilivyofaa kupelekwa katika Ikulu ya White House.
Sumu iliyonyunyiziwa barua hiyo ilitokana na aina fulani ya maharagwe yanayojulikana kama caster beans.
Ikulu ya White House haijatoa taarifa yoyote kuhusiana na barua hiyo iliyotumwa na watu wasiojulikana.
Idara ya Upelelezi ya nchini Amerika (FBI) na maafisa wa Ulinzi wa Rais (Secret Service) wameanzisha uchunguzi ili kubaini watu waliotuma barua hiyo hatari.
Majasusi pia wanalenga kubainisha ikiwa watu hao pia walitumia watu wengine barua zenye sumu.
“Kufikia sasa hatujui ikiwa barua hiyo ilitumwa kwa wanasiasa wengine au la,” idara ya FBI ikaambia vyombo vya habari vya Amerika.
Gazeti la New York Times liliripoti kwamba maafisa wa uchunguzi wanaamini kuwa kifurushi hicho kilitumwa kutoka Canada.
Polisi wa Canada Jumamosi walisema kuwa wanashirikiana na FBI kufanya uchunguzi ili kuwanasa watu waliotuma barua hiyo.
Maharagwe hayo hutoa sumu inayoweza kusababisha kuharibika kwa viungo ndani ya mwili inapomezwa au hewa yake kuvutwa kupitia puani.
Sumu hiyo inayojulikana kama ricin, inapoingia mwilini husababisha kutapika, kichefuchefu na kuvuja damu kwenye mwili.
Mtu anapomeza sumu hiyo anaweza kufariki kati ya saa 36 na 72 kulingana na kiasi cha sumu kilichoingia mwilini, kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Amerika (CDC).
“Ricin ni sumu hatari sana. Inapoingia mwilini hufululiza hadi kwenye seli za mwili na kuzizuia kupata protini. Bila protini seli hufa na hatimaye mwili wote hufa,” kikasema kituo cha CDC.
CDC inasema kuwa sumu ya maharagwe hayo imekuwa ikitumiwa katika mashambulio ya kigaidi.
Hiyo si mara ya kwanza kwa kifurushi chenye sumu kutumwa katika Ikulu ya White House na taasisi nyinginezo za serikali ya Amerika.
Mnamo 2014, mwanaume kutoka jimbo la Mississippi alihukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani kwa kutumia Rais Mstaafu Barack Obama na maafisa wengine wa serikali barua iliyokuwa na unga wa sumu ya ricin.
ya Amerika iliharamisha sumu hiyo mnamo Julai, mwaka jana.
Mnamo 2018, aliyekuwa afisa wa jeshi la majini wa Amerika alishtakiwa kwa kutuma barua zilizokuwa na sumu hiyo kwa makao makuu ya jeshi, Pentagon, na Ikulu ya White House.