Kimataifa

Wenye makalio makubwa hawawezi kugonjeka kisukari – Utafiti

November 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA na PETER MBURU

UTAFITI mpya umeonyesha kuwa watu walio na unene katika sehemu za miguu, mapaja na makalio wanaweza kuwa katika kiwango cha chini cha hatari ya kupata magonjwa ya sukari na mshtuko wa moyo.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Cell Research ulionyesha kuwa kukosa mafuta katika sehemu za chini za mwili huenda pamoja na kuongezeka kwa hatari ya kifo ama kupata magonjwa hayo.

Hata hivyo, utafiti huo hauwezi kutumika kwa wale walio na uzito katika mwili mzima, kwani kuwa na mafuta mengi katika sehemu za juu za mwili kama mbavu na moyo ni hatari kwa afya.

Akitoa matokeo ya utafiti huo, mtafiti mkuu Dkt Norbert Stefan, mtaalamu katika ugonjwa wa sukari alisema kuwa ni vyema watu kuwa na muundo wa kunenepa chini na kukonda juu wa mwili badala ya kinyume chake ikiwa uzani wao wa mwili ni mzuri kiafya kwakuwa makalio na mapaja yanahifadhi mafuta.

Utafiti huo ulisema kuwa uzani wa ziada katika sehemu hizo si sawa na ule wa ziada katika sehemu za juu za mwili. Kuwa na mafuta katika sehemu za juu za mwili kunahatarisha kuchafua damu, jambo linaloweza kusababisha ugonjwa wa sukari.