WHO yatoa mapendekezo kupunguza idadi ya wagonjwa wa TB
KILA siku zaidi ya watu 3,400 ulimwenguni hufariki kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu na wengine 30,000 wakiambukizwa.
Mwaka 2023, watu 10.8 milioni waliugua kifua kikuu huku 1.25 milioni wakiaga dunia kutokana na maradhi hayo hatari.
Ulimwengu unapoadhimisha Siku ya Kifua Kikuu (TB) Jumatatu ijayo (Machi 24), Shirika la Afya Duniani (WHO) linahimiza wadau kuwekeza zaidi na kutekeleza mikakati waliyoahidi ili kuzuia na kupunguza idadi ya vifo.
WHO inarai umma kujifunza kuhusu dalili, chanzo na jinsi ugonjwa huu unavyozuiwa, kutoamini habari zisizo za ukweli kuhusu TB na kusimama imara dhidi ya unyanyapaa kwa wagonjwa.
Kwa wahudumu wa afya, WHO inawashauri kujumuisha huduma muhimu za kifua kikuu katika huduma za kawaida za afya.
Wizara za afya na wakuu wa programu za TB wanashauriwa kutenga fedha kuboresha uchunguzi, kinga, matibabu na huduma za TB na kuzifanya ziwe thabiti na endelevu.
Pia, wameshauriwa kuwasaidia na kuwawezesha wahudumu wa afya kutoa huduma bora za TB kwa kuzingatia mapendekezo ya WHO.
Vilevile, wametakiwa kuhakikisha kuwa kuna mafunzo ya kutosha kuhusu huduma za kifua kikuu.