Kimataifa

Yaibuka fedha za kukabili Boko Haram zinafujwa

May 29th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na AFP

WANAHARAKATI nchini Nigeria Jumatatu waliishinikiza serikali ya taifa hilo kukoma kutoa mamilioni ya fedha kwa operesheni za usalama ambazo walidai kuna ukosefu wa uwazi.

Wanaharakati hao walidai kwamba kuna uwezekano kwamba fedha hizo zinatumiwa kuendeleza ufisadi kwa kisingizio cha kukabiliana na wanamgambo wa kundi la Boko Haram.

Ripoti zilisema kuwa nyingi za fedha hizo ni mapato ambayo serikali inapata kutokana na uuzaji wa mafuta.

Nigeria inakabiliwa na tishio la usalama kutoka kwa wanamgambo hao, hasa katika maeneo ya kaskazini mashariki. Juhudi za kuwakabili hazijazaa matunda, licha ya kutuma mamia ya wanajeshi kufanya misako dhidi yao.

Na kando na kuwakabili wanamgambo hao, wanajeshi pia wanakabiliwa na kibarua kingine cha kulinda visima vya mafuta dhidi ya wachimbaji haramu.

Shirika la Transparency International (TI) linakisia kwamba matumizi ya fedha hizo hayafuatiliwi kikamilifu.

Fedha hizo hutolewa kwa vikosi vya usalama ili kuvisaidia kuendesha operesheni zao bila matatizo yoyote.

Wanaharakati hao wanashikilia kwamba kutokana na uwezo wake wa kiuchumi, taifa hilo halihitaji usaidizi wowote wa kifedha kutoka mataifa ya nje.

“Tumesikia kwamba kuna fedha zaidi zitakazotolewa. Hili ni jukwaa la wazi kuendeleza ufisadi,” wakasema.