Kimataifa

Zimbabwe si kama Kenya, Mnangagwa amuonya Chamisa

September 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA NA PETER MBURU

HARARE, ZIMBABWE

CHAMA tawala cha Zimbabwe Zanu PF kinachoongozwa na Rais Emmerson Mnangagwa (pichani) kimetoa onyo kali kwa kiongozi wa upinzani nchi hiyo Nelson Chamisa asithubutu kujiapisha kama alivyotishia, akiambiwa huko sio Kenya.

Chama hicho kilitoa madai kuwa Bw Chamisa anashauriwa kufanya hivyo na kiongozi wa ODM Raila Odinga, lakini akaonywa vikali.

Kilitaja hatua ya Bw Chamisa kutaka kujiapisha Jumamosi katika uwanja wa Highfield, Jiji kuu la Harare kuwa haramu, saa chache baada ya serikali kupiga marufuku mikutano ya umma katika jiji hilo, kwa madai kuwa ni kutokana na kusambaa kwa ugonjwa wa kipindupindu.

Akizungumza na waandishi wa habari, naibu wa katibu wa chama hicho cha uongozi Lewis Matutu alionya kuwa hali kama iliyofanyika Kenya wakati Raila Odinga alijiapisha kuwa ‘Rais wa watu’ mnamo Januari haitaruhusiwa Zimbabwe.

“Tunajua sio wafuasi wote wa MDC ambao wanaunga mkono vitendo vyake. Anataka kutatiza amani nchini na kuwapotosha vijana. Afahamu kuwa Zimbabwe sio Kenya na kuwa yeye si Bw Odinga, tunajua kuwa anapokea ushauri kutoka kwa Bw Odinga na ushauri huo hausaidii Zimbabwe,” akasema Bw Matutu.

Lakini Bw Chamisa akiwajibu alisema hata hila ya serikali kupiga marufuku mikutano ya umma haitazuia azma yao ya kujiapisha kutimia wiki hii.

Bw Chamisa alisema hatua hiyo inaashiria woga kutoka kwa Rais Emmerson Mnangagwa na sasa anajaribu kumfanya asikutane na wafuasi wake.

Kupitia msemaji wao, chama cha MDC ambacho kinaongozwa na Chamisa kilisema Zanu PF imeingiza woga kutokana na umaarufu ambao Bw Chamisa amezidi kupata

“Hizi hila za ZPR kupiga marufuku hafla kwa madai kuwa ni kwa sababu ya afya ni ishara ya woga wa ZANU PF kwa wananchi.

“Wanafahamu kuwa Mnangagwa anajua alipoteza uchaguzi na hivyo anatumia kutangazwa kwa hali ya hatari kujilinda kutokana na demokrasia,” akasema Bw Mafume.