Kiraitu, Linturi kulinda Meru 'isivamiwe' kisiasa
Na DAVID MUCHUI
VIONGOZI wa kisiasa katika Kaunti ya Meru wameapa kulinda eneo hilo dhidi ya ‘uvamizi’ wa wapinzani wao, huku wakiahidi kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022.
Wakihutubu Ijumaa kwenye mahafala katika Taasisi ya Kitaifa ya Kiufundi ya Meru, Gavana wa Meru Kiraitu Murungi na Seneta Mithika Linturi, waliwaomba wanasiasa ambao wametangaza kuwania urais kuwaheshimu viongozi wa eneo hilo ili kuwapa nafasi ‘kukamilisha kazi zao’.
Dkt Ruto alikuwa mgeni wa heshima katika hafla hiyo ambapo wanafunzi 1,125 walifuzu kwenye taaluma mbalimbali.
Kwenye kauli zilizoonekana kupinga ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI), wawili hao walisema kwamba watawashinikiza viongozi wengine kubuni msimamo thabiti kuhusu utatuzi wa changamoto zinazoathiri eneo hilo.
Wakirejelea matokeo ya uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra, walisema kuwa kuna haja ya viongozi kuheshimu mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo.
Data za sensa
Bw Linturi alisema kuwa kulingana na matokeo ya Sensa yaliyotolewa majuzi, ni dhahiri kuwa kaunti hiyo ina idadi kubwa zaidi ya watu katika eneo hilo.
“Kama tunavyoheshimu misimamo ya kisiasa ya maeneo mengine, msimamo wetu pia unapaswa kuheshimiwa. Tunapaswa kupewa nafasi ya kufanya maamuzi yetu kwa njia huru ili kujua vile tutafanya kazi na viongozi wengine. Kwa kuwa Naibu Rais huwa anazuru eneo hili sana, tutakubaliana kuhusu mwelekeo wa kisiasa tutakaochukua,” akasema Bw Linturi.
Bw Murungi aliunga mkono kauli hiyo, akisema kuwa atawashinikiza viongozi wa eneo hilo kubuni msimamo huru kuhusu ripoti hiyo.