Kitui, Makueni zachukua hatua kudhibiti hatari ya mamba,viboko
KAUNTI za Kitui na Makueni zimeripotiwa kuwa na ongezeko la visa vya wakazi kushambuliwa na mamba na viboko, hasa katika maeneo yanayopakana na Mto Athi.
Mashambulizi haya yamekuwa tatizo kila mwaka, yakiua na kusababishia wakazi na mifugo majeraha.
Serikali za kaunti zimechukua hatua kadhaa za kupunguza hatari hizi na kuhakikisha upatikanaji salama wa maji.Moja ya mbinu muhimu ni miradi ya kupiga maji kwa pampu kutoka mtoni.
Katika Kaunti ya Kitui, Gavana Julius Malombe amekamilisha mradi wa Athi-Kangu Kangu, ambao ni ushirikiano wa miaka 12 na shirika la World Vision International.
Mradi huu unajumuisha kisima cha maji, vituo viwili vya kusafisha maji, mabomba ya kilomita 224 na matangi 13 ya kuhifadhi maji. Kwa kuweka mfumo huu, wakazi hawahitaji tena kwenda mtoni kuchota maji, hatua inayopunguza hatari ya mashambulizi ya mamba.
Kaunti ya Makueni pia inatekeleza miradi ya maji, kama Athi-Tunguni, ingawa imecheleweshwa kutokana na upungufu wa ufadhili. Miradi hii inalenga kuhudumia vijiji ambavyo hatari ya mashambulizi ya mamba ni kubwa zaidi.
Ufanisi wa miradi hii unategemea ufadhili na usimamizi mzuri wa miundombinu ya maji.
Mbinu nyingine ni kuhamasisha wananchi kuhusu hatari za mamba na viboko. Serikali za kaunti zinahimiza wananchi kutoishi au kulima kando ya kingo za mto, ambazo ni maeneo hatari.
Aidha, kaunti zimeweka usimamizi wa mazingira na mashirika ya dharura. Takwimu kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya zinaonyesha kuwa eneo la mpaka wa Kaunti za Kitui na Makueni, hupoteza zaidi ya watu 10 kila mwaka kutokana na mashambulizi ya mamba na viboko.
Kuwa na vikundi vya dharura na mifumo ya tahadhari ya mapema kunasaidia kupunguza vifo na majeruhi.Hatua hizi, zinazojumuisha miradi ya maji, elimu ya jamii, ulinzi wa kingo za mito, na usimamizi wa dharura, zinaonyesha jitihada za kaunti za Kitui na Makueni kupunguza hatari ya mashambulizi ya mamba.
Hata hivyo, ufanisi wake unategemea mshikamano wa jamii, ufadhili thabiti, na ufuatiliaji endelevu wa miradi ya maji na usalama wa mazingira.
