Habari

KNH: Wauguzi washtakiwa kumuua mgonjwa wa kansa kinyama

May 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE alibubujikwa na machozi Jumatatu aliposimulia jinsi  alikuta maiti ya mumewe imelazwa katika kitanda kilichokuwa na damu jingi kwenye Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH).

Bi Celestine Mwenda alimweleza Jaji James Wakiaga kuwa mumewe aliuawa na watu wasiojulikana KNH alipokuwa amelazwa kutibiwa ugonjwa wa saratani.

Akisimulia kuhusu kisa hicho kilichotokea miaka miwili unusu iliyopita, Bi Mwende alisema alimtembelea mumewe Cosmas Mutunga kila siku lakini mnamo Novemba 28, 2015 alimkuta ameuawa huku kichwa chake kikiwa kimebondwa na macho kutolewa!

“Kitanda alichokuwa amelalia mume wangu kilikuwa kimelowa damu . Nilikuwa nimemwacha akiwa mwenye furaha mwendo wa saa moja usiku Novemba 27, 2015,” akasema shahidi huyo.

Lakini siku iliyofuata, alirudi hospitalini na kupigwa na butwaa kuona maiti ya mumewe imefunikwa blanketi yenye damu akiwa ameaga.

Alisema hayo alipotoa ushahidi dhidi ya wauguzi wanne wanaoshtakiwa kumuua Bw Mutunga.

Wauguzi hao Bi Priscilla Wanjiru Njeru, Bw Godfrey Murithi Gachora, Bi Rosemary Nkonge na Mary Muthoni wameshtakiwa kumuua kinyama Bw Mutunga.

Kesi inaendelea.