Koma kujitangaza msemaji wa Mlima, Waiguru aambia Gachagua
GAVANA wa Kirinyaga, Anne Waiguru, amemlaumu aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, kwa kujitwika wadhifa wa kiongozi wa Mt Kenya na kuwaonya wakazi wasimfuate kama vipofu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi wa Chuo cha Mafunzo ya Utabibu katika Kirinyaga Central mjini Kerugoya, Gavana Waiguru alishangaa ni nani alimteua Gachagua kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya.
“Ni nani alimteua Gachagua kuwa Mfalme wa Mlima?’ alihoji.
Aliwakumbusha wakazi kwamba Rais mstaafu Uhuru Kenyatta bado ndiye msemaji wa eneo hilo lenye wapiga kura wengi.
“Ni Kenyatta aliyepewa jukumu la kuongoza Mlima na hatujampokonya wadhifa huo, Gachagua asijigambe kuwa ndiye msemaji wa eneo letu,” alisema Gavana Waiguru.
Alidai kwamba Gachagua amepoteza umaarufu katika eneo hilo kwa kudharau viongozi waliochaguliwa.’Watu wanapokataa chama chake, Democracy for Citizens Party (DCP), ni kwa sababu mwanzilishi wake sasa hana umaarufu,’ alisema.
Gavana Waiguru pia alikanusha madai kwamba angeacha chama cha UDA kujiunga na chama cha Gachagua.
“Ni ukweli tu, siwezi kujiunga na Wamunyoro, siwezi kwenda huko,” alisema.
Akiandamana na Mbunge wa Kirinyaga Central, Gachoki Gitari, Gavana Waiguru aliwahimiza wakazi wa Mlima Kenya kusalia katika serikali ili wafurahie maendeleo.
Alisema Gachagua hana maendeleo ya kuwapa wakazi, na wanapaswa kumkubali Rais William Ruto na serikali ili wawe sehemu ya maendeleo ya kitaifa.’Gachagua hana wadhifa serikalini, hana nafasi ya kuchaguliwa, na hatuwezi kumtegemea, wacha tumsahau na tufanye kazi na serikali,’ alisema.