Habari

Korti yatoa agizo TSC iendelee kushirikiana na Knut

November 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Leba, iliamuru Ijumaa kwamba Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) inafaa iendelee kushirikiana na Chama cha Kitaifa cha Kutetea Walimu (Knut).

Jaji Byram Ongaya aliamuru TSC iwasilishe sababu za kutotambua Knut, chama kilichosajiliwa miaka 51 iliyopita.

Wakili Judy Gusera anayekiwakilisha Knut alimweleza Jaji Ongaya kwamba chama hicho kinakabiliwa na tisho ya kusambaratishwa na TSC.

“Kumekuwa na mizozo tele kati ya TSC na Knut kinachotetea haki za walimu. Kitovu cha mizozo hii ni tisho kwamba TSC itatamatisha uhusiano wake na chama hiki. TSC hukata ada ya kiwango fulani cha pesa zinazopelekewa Knut kuendeleza shughuli zake,” Bi Guserwa alimweleza Jaji Ongaya.

Mahakama iliambiwa TSC imekipa Knut muda wa miezi miwili kupata idadi inayofaa ya wanachama ndipo ushirikiano uliopo uendelee.

Jaji Ongaya alielezwa kwamba hatua hii ya TSC inakaidi katiba na kukandamiza haki za walimu nchini.

“Katiba ya nchi hii inawakubalia wafanyakazi kujiunga na chama cha kutetea haki zao,” alisema Bi Guserwa na kuongeza ni jambo la kustaajabisha kwa TSC kutoa makataa ya miezi miwili kwa Knut kuwa na idadi ya wanachama wake inayotaka la sivyo ikomeshe ushirika uliopo.

Bi Guserwa alimweleza Jaji Ongaya kuwa iwapo TSC itatekeleza tisho lake, basi walimu zaidi 200,000 watakosa chama cha kuwatetea.

Ushahidi

Baada ya kuratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura, Jaji Ongaya alimwamuru Bi Guserwa kukabidhi TSC nakala ya kesi hiyo ndipo iwasilishe ushahidi kuhusiana na madai ya Knut.

Katika siku za hivi punde TSC imekabana koo na katibu mkuu wa Knut na hata kupelekea kuondolewa kwa jina la Bw Wilson Sossion kutoka orodha ya walimu.

Bw Guserwa alieleza korti mzozo kati ya TSC na Knut umezua hisia kali na kwamba haki za walimu zitaathirika pakubwa endapo mahakama haitaingilia kati na kutoa suluhu.

“Nimesoma kesi iliyowasilishwa na Knut pamoja na mawasilisho ya wakili Guserwa na kufikia uamuzi kuna masuala mazito ya kisheria yanayopasa kuamuliwa,” alisema Jaji Ongaya.

Jaji huyo aliamuru kesi hiyo isikizwe Novemba 19, 2019.