Kwa nini Kanyari alipewa haki ya kuwalea watoto waliompendelea baba mlezi
MAHAKAMA ya hakimu imeamua kuwa mhubiri Victor Kanyari ndiye anayestahili kupewa haki ya kisheria ya kuwalea watoto wake wawili aliozaa na mwimbaji wa nyimbo za injili marehemu Betty Bayo, licha ya watoto hao kutaka kuendelea kuishi na baba yao wa kambo, Hiram Gitau, maarufu Tash.
Hakimu Casmir Obiero aliamua kuwa Kanyari alitoa hoja zenye nguvu zaidi kwa kuwa ndiye mzazi wao wa kuwazaa aliye hai. Hata hivyo, mahakama iliagiza watoto hao wasihamishwe mara moja kutoka kwa Tash, bali mchakato wa kuwapeleka kwa baba yao ufuate mpango maalumu unaozingatia hisia na masomo yao.
Bayo alifariki Novemba 10, 2025, na watoto wakaendelea kuishi na Tash, ambaye alisema amekuwa akiwalea tangu 2020.
Watoto hao, wenye umri wa miaka 13 na 10 walipotoa ushahidi, waliambia mahakama kuwa wanataka kubaki na Tash, ambaye wamezoea kumtegemea tangu mama yao afariki. Walieleza pia wasiwasi kuhusu kuishi na baba yao mzazi.
Mahakama ilisema maoni ya watoto ni muhimu chini ya Kifungu cha 103 cha Sheria ya Watoto, lakini hayaamui kesi peke yake.
Ripoti ya afisa wa watoto ya Agosti 20 ilionyesha kuwa watoto hao wamefungamana kihisia na Tash na kupendekeza mawasiliano yao na Kanyari yaanzishwe hatua kwa hatua.
Afisa wa watoto wa Kiambu alipewa siku 14 kuandaa mpango wa mpito, ukizingatia masomo, usafiri, ustawi wa kihisia na mawasiliano na wanaume hao wawili. Ripoti ya utekelezaji inapaswa kuwasilishwa mahakamani ndani ya siku 30.
Kanyari aliambia mahakama kuwa amekuwa akichangia mahitaji ya watoto, yakiwemo karo, mavazi, chakula, matibabu na safari. Alisema ana nyumba Runda, Ruai, Daykio na Njiru ambako anaweza kuwalea.
Tash naye alisema amekuwa akiwatunza watoto hao, akihudhuria mikutano ya shule na kugharamia elimu na mahitaji yao ya kila siku.
Hata hivyo, mahakama ilikataa madai yake ya kuwa mume wa Bayo chini ya mila za Wakikuyu, ikisema picha za sherehe hazikuthibitisha ndoa hiyo. Hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu mahari, mazungumzo ya ndoa, taratibu za kimila au mashahidi.
Hakimu pia alisema Tash hakuwa amepata haki ya kisheria ya kuwa mzazi kupitia kuasili watoto au taratibu nyingine rasmi.
Mahakama iliamuru wanaume hao wawili waendelee kutimiza mahitaji ya watoto bila kutegemea nani ana haki ya kuwalea. Kanyari ataruhusiwa kuwasiliana nao mara kwa mara na kuwaona kila baada ya wikendi moja.
Pia, hakuna atakayeruhusiwa kuwatoa watoto nchini, kuwahamisha shule au kuwahamisha nje ya mamlaka ya mahakama bila makubaliano ya maandishi au ruhusa ya mahakama.