HabariHabari za Kitaifa

Mkenya anayefanya kazi katika serikali ya Trump akamatwa kwa kuishi Amerika kinyume cha sheria

Na HILARY KIMUYU October 29th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MKENYA anayefanya kazi katika idara ya serikali ya jimbo la Washington inayoshughulikia ustawi wa watoto na familia amekamatwa na maafisa wa uhamiaji wa Amerika kwa madai ya kuishi nchini humo baada ya muda wa visa yake kuisha.

Stanley Robert Kungu Muthee alikamatwa na maafisa wa Huduma ya Uhamiaji na Forodha (ICE) wakati wa ukaguzi wa barabarani Jumatatu, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na idara hiyo kwa kituo cha Fox News.

ICE ilisema Muthee aliingia Amerika Februari 6, 2019, kwa visa ya utalii aina ya B-2 lakini hakurejea nyumbani baada ya muda aliokuwa ameruhusiwa kukaa humo kuisha.

“Aliingia Amerika kwa mara ya kwanza Februari 6, 2019, kwa visa ya utalii lakini hakuwahi kuondoka na akaendelea kukaa nchini humu kinyume cha sheria,” ICE ilisema.

Kukamatwa kwake kunajiri wakati utawala wa Rais Donald Trump umeimarisha msako dhidi ya wahamiaji wasio na vibali halali.

Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika imesema zaidi ya visa 300,000 zimebatilishwa katika hatua hiyo.

ICE ilisema Muthee alikiri kufanya kazi katika Idara ya Watoto, Vijana na Familia ya Washington (DCYF). Wakati wa kukamatwa, alikuwa amevaa koti lenye jina la idara hiyo na alikuwa na kitambulisho cha kazi.

Hata hivyo, DCYF ilisema Muthee aliajiriwa Agosti 16, 2024, baada ya kuwasilisha stakabadhi zilizoonyesha kuwa alikuwa na ruhusa ya kufanya kazi Amerika.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa idara hiyo, Nancy Gutierrez, alisema hawakuwa wamejulishwa kuhusu mabadiliko yoyote katika hali yake ya uhamiaji.

Alisema stakabadhi alizowasilisha zilijumuisha nambari halali ya Huduma za Uraia na Uhamiaji ya Amerika (USCIS), ambayo haikuwa na tarehe ya kuisha.

Kesi yake inaibua maswali kuhusu tofauti kati ya kibali cha  kufanya kazi Amerika na kuwa na hadhi halali ya uhamiaji. Kibali cha kufanya kazi hakihakikishi moja kwa moja kuwa mtu ana haki ya kuendelea kuishi nchini humo.

Kukamatwa kwa Muthee pia kunajiri wakati ambapo hifadhidata ya Wizara ya Usalama wa Ndani ya Amerika (DHS) imeorodhesha angalau Wakenya 52 waliokamatwa na ICE katika majimbo mbalimbali.

Orodha hiyo inajumuisha watu wanaohusishwa na makosa mbalimbali, yakiwemo mauaji, wizi, ulaghai, makosa ya kingono na ukiukaji wa sheria za uhamiaji.

Hata hivyo, kukamatwa hakumaanishi moja kwa moja kuwa mtu amepatikana na hatia. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kuhusu Muthee, msingi wa kukamatwa kwake ni madai ya kuishi Amerika baada ya muda wa visa kuisha. Hakuna hukumu ya jinai dhidi yake iliyotajwa katika taarifa hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika, Tommy Pigott, alisema utawala wa Trump umebatilisha visa zaidi ya 300,000, akidai kuwa hakuna utawala mwingine uliowahi kufanya hivyo kwa kasi hiyo.

“Uamuzi wowote wa kutoa visa ni uamuzi unaohusu usalama wa taifa, na wajibu huo haukomi baada ya visa kutolewa,” alisema.

Aliongeza kuwa ukiukaji wa sheria au vitisho kwa usalama wa taifa vinaweza kuwa sababu za kubatilisha visa.

DCYF inashughulikia masuala ya ulinzi wa watoto, malezi, kuasili watoto na huduma kwa familia zilizo katika mazingira magumu.

Idara hiyo haikufafanua cheo cha Muthee wala iwapo kazi yake ilihusisha kukutana moja kwa moja na watoto.

Bado haijabainika iwapo Muthee aliwahi kutuma ombi la hifadhi ya ukimbizi, kupata hadhi nyingine ya uhamiaji au kutafuta njia nyingine ya kuruhusiwa kuishi Amerika.

ICE pia haikutoa maelezo zaidi kuhusu hatua zinazofuata katika kesi yake ya uhamiaji.