Habari

Lawama kwa Lapsset uhaba wa maji safi na salama Lamu

March 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

BODI ya Kusambaza Maji, Kaunti ya Lamu (Lawasco) imenyooshea kidole cha lawama ujenzi unaoendelea wa mradi wa Bandari ya Lamu (Lapsset) kwa kusababisha uhaba mkubwa wa maji ambao umekuwa ukishuhudiwa kwenye baadhi ya miji eneo hilo siku za hivi karibuni.

Wiki iliyopita, mamia ya wakazi wa mji wa Mokowe na viungani mwake waliandamana barabarani na kufululiza hadi ofisi za Lawasco na pia makao makuu ya Kaunti ya Lamu mjini Mokowe kushinikiza serikali ya kaunti kutatua tatizo la maji walilodai limedumu eneo hilo kwa zaidi ya muda wa miezi mitano.

Katika mahojiano na ‘Taifa Leo’ ofisini mwake, Meneja wa Lawasco, Bw Paul Wainaina amesema Jumatano tangu mradi wa ujenzi wa Lapsset kuanzishwa eneo hilo, visima vingi vimeishia kukauka ilhali vingine maji yake yamegeuka kuwa ya chumvi kutokana na kutumiwa sana kwenye ujenzi huo unaojumuisha viegesho vitatu vya kwanza vya Lapsset.

Bw Kimani amesema tangu jadi, miji mingi ya Lamu, ikiwemo Mokowe, Hindi na viunga vyake, imekuwa ikitegemea maji ya visima ambavyo vilichimbwa tangu miaka ya 1990.

Alisema ujio wa Lapsset umesababisha maji mengi kupita kiasi kutumiwa kutoka kwa visima hivyo ili kutekelezea ujenzi wa mradi huo, hatua ambayo sasa imechangia kukauka kwa visima hivyo ilhali vingine vikitoa maji ya chumvi ambayo hayawezi kutumiwa na binadamu.

“Ninakubali malalamishi ya wakazi kwamba miji yao haina maji, lakini Lawasco inajitahidi kufikisha maji majumbani,” akasema Bw Wainaina.

Akaongeza: “Isitoshe, miji kama vile Mokowe tangu jadi imekuwa ikitumia maji ya visima. Tangu ujenzi wa viegesho vitatu vya Lapsset kuanza, visima hivyo pia vimekuwa vikitegemewa kusambaza maji ya kutekelezea ujenzi huo. Hii ndiyo sababu visima vingi vimekauka ilhali vingine vikitoa maji ya chumvi kutokana na kutumiwa sana kupita kiasi.”

Afisa huyo aidha amesema serikali ya Kaunti ya Lamu iko mbioni kuchimba visima vipya kwenye maeneo mbalimbali ya Lamu, ikiwemo Belebele na Hongwe ili kusaidia kukabiliana na uhaba huo wa maji unaokumba wakazi.

Amesema kaunti kwa ushirikiano na wafadhili mbalimbali na serikali kuu pia wako mbioni kujenga mitambo ya kusafisha maji ya chumvi na kuyagauza kuwa safi kwa matumizi ya binadamu katika harakati zake za kukabiliana na uhaba wa maji Lamu.

Bw Wainaina aidha ameisihi serikali kuu kutoa fedha za kusaidia katika usawa na maendeleo ya maeneobunge (Equalisation Funds) ili kusaidia kutekeleza miradi hiyo ya maji eneo la Lamu.

“Mbali na kuchimba visima, kaunti ikishirikiana na wafadhili mbalimbali pamoja na serikali kuu pia wako na mpango wa kuanzisha mitambo ya kusafisha maji ya chumvi kutoka Bahari Hindi ili yawe safi kwa matumizi ya binadamu. Ombi langu kwa serikali kuu ni kwamba waharakishe utoaji wa fedha za usawa na maendeleo ya maeneo bunge ili kusaidia kufaulisha miradi yetu ya maji hapa Lamu,” amesema Bw Wainaina.