LSK yalalamika polisi wananyanyasa mawakili
CHAMA cha Wanasheria Nchini (LSK) kimelaumu polisi kwa kuwanyanyasa na kuwatisha mawakili, hatua ambayo kimeirejelea kama njama ya kuwasukuma wateja wao ili kufanikisha matokeo fulani katika kesi.
Rais wa LSK, Faith Odhiambo, kupitia taarifa Jumatano, Mei 28 2025, alilalamika kuwa baadhi ya mawakili wamekuwa wakilengwa na mbinu za vitisho ambazo alisema ni sehemu ya mpango mpana wa kudhoofisha uwakilishi wa kisheria na kuzuia upatikanaji wa haki.
Bi Odhiambo alionya kuwa hatua kama hizi zinaweza kugeuza Kenya kuwa taifa la kiimla linalopuuza haki za binadamu na uhuru wa raia.
Alisisitiza umuhimu wa kulinda Katiba na utawala wa sheria.
“Mwelekeo wa kutisha umeibuka ambapo mawakili wanatishwa kama sehemu ya njama ya kuwanyanyasa wateja wao,” alisema Bi Odhiambo, akiongeza kuwa hii ni mbinu ya zamani lakini inayolenga kukandamiza uhuru, na haina nafasi katika mfumo wa sheria wa Kenya.
“Polisi hawapaswi kuvuka mpaka ulio wazi uliowekwa na Katiba katika kutetea haki na utawala wa sheria. Hatupaswi kurudi nyuma kwa maagizo yasiyo halali au juhudi zisizo na msingi wa kisheria,” aliongeza.
Alikemea vikali tabia ya maafisa wa polisi kujitokeza usiku katika makazi ya mawakili, akisisitiza kuwa mawakili wanapaswa kuitwa kupitia njia rasmi na halali iwapo inahitajika watoe taarifa. Alitoa wito kwa polisi kuheshimu mipaka ya sheria.
Bi Odhiambo aliwataka polisi kuacha mara moja tabia hii , akisisitiza kuwa ni jambo lisilokubalika na linafaa kusitishwa ili kulinda heshima ya mfumo wa haki wa Kenya na haki za wanasheria pamoja na wateja wao.
Hata hivyo, Bi Odhiambo hakutoa maelezo ya kina kuhusu mawakili waliovamiwa na polisi majumbani mwao.
Mnamo mwezi Aprili mwaka huu, LSK iliandika barua kali kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhusu kile ilichotaja kama kukamatwa kiholela na kunyanyaswa kwa wanachama wake.
Katika barua hiyo, Mwenyekiti wa Tawi la Nairobi, Eric Kivuva, alilaani vikali hatua za maafisa wa Kituo cha Polisi cha Kasarani na DCI waliodaiwa kumhangaisha wakili aliyekuwa akitekeleza majukumu yake ya kisheria.
“Tawi la Nairobi linalaani vikali kabisa vitendo vya DCI na Polisi wa Kasarani, ambavyo ni unyanyasaji na vitisho kwa wakili katika utekelezaji halali wa kazi yake,”ilisema sehemu ya barua hiyo.