Maandamano ya wanahabari yashika kasi nchini
NAIROBI
WANAHABARI kote nchini waungana pamoja na kuandamana barabarani kulalamikia kunyanyaswa na kudhulumiwa na maafisa wa polisi.
Aidha, walikuwa wakitaka serikali kuwajibika ndiposa haki ipatikane kwa mwanahabari wa kike wa runinga ya Kameme, Catherine Wanjeri Kariuki aliyemiminiwa risasi tatu pajani akiwa kazini siku ya maandamano ya Gen Z wiki jana, katika jiji la Nakuru.
Wanahabari hao pia walikashifu vitendo vya maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia kwa kuwarushia wanahabari vitoza machozi, maji yalio na muasho na kutuia bunduki zao kuwalenga wanahabari.
Hapa jijini Nairobi, waandamanaji walikusanyika saa nne nje ya Jumba la Nation mkabala wa barabara ya Kimathi.
Walibeba mabango yaliyoandikwa jumbe mbalimbali zilizoashiria kupaaza sauti kwao ili serikali iwasikie.
Wengine walipuliza firimbi, kua wale waliopuliza vuvuzelana wengine kubeba bendera kadhaa za taifa.
Kwa mara ya kwanza na ya kihistoria, wanahabari waliongozwa na gari la polisi lililokuwa na kamanda wa cheo cha Superiteni Mkuu.
Walitembea hadi makutano ya barabara ya Moi na Haile sellasie na kusimama kuimba wimbo wa Taifa.
Baadaye waliandamana hadi kwa ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi katika Jumba la Jogoo.
Kutoka hapo walielekea katika makao makuu ya Polisi kabla ya kuelekea katika ofisi ya waziri wa masuala ya ndani na usalama wa Taifa katika jumba la Harambee.
Baadaye, walielekea katika bunge la Taifa wakisisitiza kuongea na spika Moses Wetangula lakini spika hakuwepo.
Baada ya Bunge waliandamana katika barabara ya Bunge, ya Cathedral hadi ya Kenyatta na kusimama nje ya Jumba la Teleposta kutaka kuongea na waziri wa Masuala ya Teknolojia.
Kilele cha maandamano mwendo wa saa saba unusu kilikuwa kurudi nje ya Jumba la Nation ambapo mahojiano ya waathiriwa, viongozi yalifanyika kabla ya washiriki kutawanyika kurudi katika vyumba vyao vya habari mtawalia.