Maaskofu na mapadri hunyemelea watawa kimapenzi – Papa Francis
Na MASHIRIKA
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki ulimwenguni, Papa Francis amekiri watawa wengi wamekuwa wakidhulumiwa kimapenzi na mapadri na maaskofu.
Hii ni sakata nyingine inayohusu dhuluma za ngono katika kanisa hilo ambalo limekuwa likikumbwa na kashfa tele za wahubiri wake kulawiti watoto wa kiume.
Akizungumza Jumatano akiwa safarini kwenye ndege yake kutoka ziara ya Milki ya Kiarabu (UAE) kuelekea Vatican, Papa Francis alisema makao makuu ya Kanisa Katoliki yalipokea ripoti kuhusu mapadri wanaodhulumu watawa hapa Afrika katika miaka ya tisini, na kuongeza kuwa tatizo hilo bado lipo hadi sasa hasa katika makanisa mapya.
“Kuna mapadri na hata maaskofu ambao wamewahi kufanya hivyo. Nadhani ni kitu ambacho kingali kinaendelea kwa sababu hiki si kitu ambacho huisha tu ghafla, la hasha!” akasema.
Aliongeza: “Sitaki kusikia ikisemekana kwamba kanisa halina tatizo hili, kwa sababu ukweli ni kuwa lipo. Tunahitajika kujitahidi zaidi kulikomesha na tuna nia ya kufanya hivyo.”
Alisema hayo alipoulizwa swali kuhusu ripoti iliyochapishwa majuzi kwenye jarida la ‘Women Church World’ ambalo husambazwa na gazeti la Osservatore Romano linalochapishwa Vatican.
Ripoti hiyo ilifichua jinsi watawa wamekuwa kimya kuhusu dhuluma ambazo wamekuwa wakipitia kwa miongo mingi mikononi mwa maaskofu na mapadri kwa sababu wanaogopa kuadhibiwa wwakifichua.
Suala hilo liligonga vichwa vya habari mwaka uliopita baada ya mtawa kudai askofu wa kanisa lililo nchini India alimbaka mara kadhaa.
Katika kisa hicho, Askofu Franco Mulakkal wa miaka 53, alikamatwa Septemba 21 kwa kushukiwa kumbaka mtawa huyo mara 13 kati ya mwaka wa 2014 na 2016. Papa Francis alimsimamisha kazi kwa muda siku moja kabla akamatwe.
Nchini Kenya, kumekuwa na kashfa tele katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu madai ya ubakaji na ulawiti unaotendwa na viongozi wa kanisa hilo. Kisa cha majuzi kiliripotiwa Kiambu ambapo padri alidaiwa kushiriki ngono na wasichana wachanga waumini na pia kuwasaidia kuavya mimba.
Mwaka uliopita, shirika la International Catholic Organisation lilitoa wito kwa akina mama wenye watoto ambao baba zao ni mapadri wajitokeze ili watoto hao wafanyiwe uchunguzi wa DNA kwa ajili ya kufanya baba zao wawajibikie ulezi wao.
Papa Francis alisema kuna viongozi wengi wa kidini katika kanisa hilo ambao wamesimamishwa kazi kwa kudhulumu watawa na afisi yake imekuwa ikijitahidi kusuluhisha tatizo hilo kwa muda mrefu.
Kulingana naye, tatizo lenyewe ni la kidesturi lililo na mizizi yake katika jinsi wanawake wanavyotazamwa kuwa wasio na thamani katika jamii.
Alitoa mfano wa kisa kilichotokea Ufaransa ambapo mtangulizi wake, Papa Benedict wa 16 alijaribu kuchukua hatua lakini juhudi zake zikazimwa na baadhi ya maafisa wakuu wa Vatican:
Kumekuwa na mapendekezo kuwa Kanisa Katoliki liwaruhusu mapadri wake kuoa.