Macho kwa Sifuna akipigwa vita ODM
KATIBU Mkuu wa chama cha ODM, Bw Edwin Sifuna, anapigwa na mawimbi ya kisiasa huku chaguo zake zikizidi kupungua akikabiliana na Rais William Ruto na vigogo wa ODM wanaounga mkono azma ya rais kuchaguliwa tena.
Seneta huyo wa Nairobi ameongeza mashambulizi yake dhidi ya serikali jumuishi baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga, hali inayomfanya kuonekana kana kwamba anajitenga polepole na chama chake.
Bila kuonyesha dalili ya kubadili msimamo, Sifuna, 43 na Naibu Kiongozi wa Wachache katika Seneti, anaogelea katika mawimbi yanayoweza kuamua hatima yake ya kisiasa kabla ya uchaguzi ujao.
Ingawa Bw Sifuna ana chaguo kadhaa kisiasa, hakuna unaonekana kuwa rahisi.
Akiwa mkosoaji mkali wa wazo la ODM kuunga mkono rasmi azma ya Rais Ruto kuchaguliwa tena mwaka 2027, amejipata katika mazingira tata ya kisiasa yaliyojaa migawanyiko ya ndani ya ODM na mabadiliko ya miungano, huku hatua yake ijayo ikitarajiwa kuwa na athari kubwa kwa mustakabali wake.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Bw Javas Bigambo, anasema Seneta Sifuna ana chaguo nyingi, baadhi zikiwa na matumaini na nyingine hatari, kutegemea jinsi anavyojipanga kisiasa.
“Ikiwa anajiona kama simba lakini hayuko katika msitu wa simba bali yuko kwenye dimbwi la kuogelea, basi atapata tabu. Kuna watu wanaompigia makofi ambao si wapigakura wa Nairobi na watamsahau haraka kama Ababu Namwamba alipoporomoka kisiasa,” alisema Bw Bigambo.
Aliongeza kuwa Bw Sifuna amekuwa wazi mno kuhusu mikakati yake ya kisiasa.
“Katika siasa, hufai kuweka karata zako zote mezani. Ni rahisi kutabiri hatua zake zinazofuata, jambo linaloashiria ukosefu wa mkakati. Wakati mwingine hekima ni kuwaacha watu wakikisia,” alisema.
Hata hivyo, Bw Sifuna anaonekana kana kwamba anataka kwa makusudi ODM imtimue, akiendelea kuichokoza kwa kauli na vitendo vinavyolazimisha chama kuchukua hatua.
Mbali na kuongoza vuguvugu la Kenya Moja, amekuwa akijihusishwa zaidi na Muungano wa Upinzani, akihudhuria mikutano yake ya hadhara na kuzua uvumi kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa.
Muungano huo wa Upinzani unajumuisha chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, ambaye Bw Sifuna amemtetea hadharani kuhusu kushindwa kwa Raila Odinga katika uchaguzi wa urais wa 2022.
Pia unajumuisha chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Wiper Patriotic Front cha Kalonzo Musyoka, miongoni mwa vingine.
Muungano wa upinzani unatarajiwa kupata uungwaji mkono mkubwa jijini Nairobi kutokana na mtindo wa upigaji kura unaozingatia misingi ya kikabila, hali inayofanya vyama hivyo kuonekana kama hifadhi ya kisiasa kwa seneta huyo anayehudumu muhula wa kwanza.
Akizungumza wakati wa mazishi ya mama wa Mbunge wa Embakasi North James Gakuya huko Murang’a Jumamosi, Bw Gachagua alidokeza wazi uwezekano wa Bw Sifuna kujiunga na upinzani.
“Tunasubiri watu wengi, akiwemo Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, ambao wanataka kujiunga nasi,” alisema Gachagua.
Katika hafla hiyo hiyo, Bw Sifuna aliwashambulia viongozi aliowataja kwa majina ambao alidai wanajaribu kumwamulia ni nani wa kushirikiana naye.
“Sitakubali mtu yeyote anichagulie marafiki au maadui, au kuniambia ni mazishi ngani ninafaa kuhudhuria. Nilichaguliwa kuwa seneta wa Nairobi na makabila yote,” alisema.
Hata hivyo, Bw Bigambo alionya kuwa Bw Sifuna lazima achunguze ikiwa ana ngome thabiti ya kisiasa.
“Ushawishi alionao ulijengwa na kuimarishwa na Raila Odinga. Haukujitokeza wenyewe. Nairobi inaweza kumgeuka mtu wakati wowote. Anaweza kuamua kufanya kazi ndani ya ODM, kuiharibu au kuondoka,” alisema.
Alionya kuwa kujiunga na watu waliokuwa wakionekana kama maadui wa kisiasa wa Bw Odinga kunaweza kuwatenga wafuasi sugu wa ODM.
“Anaweza kupigiwa makofi Mlima Kenya lakini azomwe na wafuasi wa Raila,” alisema.
Chaguo jingine kwa Bw Sifuna ni kubaki ODM na kupigania mabadiliko akiwa ndani, akitumia uungwaji mkono wa viongozi wakuu kama kiongozi wa chama Oburu Oginga na Naibu Kiongozi wa Chama Godfrey Osotsi, ambao wamemtetea.
Hii, hata hivyo, inategemea uwezo wake wa kuwashawishi wenye ushawishi ndani ya ODM kwamba mustakabali wa chama uko katika kujitenga na utawala wa Rais Ruto na kuwa na mwelekeo huru wa kisiasa.
Ukosoaji wake mkali dhidi ya serikali jumuishi unawavutia baadhi ya wafuasi wa ODM wanaohisi kutengwa na wanaomuona kama sauti ya misingi inayowatetea wananchi.
Chaguo la tatu ni kuondoka ODM kabla ya Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) uliopangwa kufanyika robo ya kwanza ya mwaka huu, na kugombea kama mgombea huru mwaka 2027.
Mnamo Agosti 2025, Bw Sifuna alidokeza kuwa atajiondoa ODM iwapo chama hicho kitamuunga mkono rasmi Rais Ruto.
Akizungumza katika hafla ya kuwawezesha wanawake Lukhome, Kaunti ya Trans Nzoia, Bw Sifuna alisema hatashiriki katika uamuzi wowote wa ODM unaomuunga mkono Rais Ruto.
Bw Bigambo alionya kuwa ingawa Bw Sifuna ni mwanasiasa mwenye busara, anahitaji kuongozwa na mkakati na kiasi.
“Anaonekana tayari kujitengenezea maadui ndani ya ODM na anajiona kama mkubwa kuliko chama,” alisema.