Madaktari, wahudumu wa afya kupigwa faini Sh1 milioni wakidhulumu mgonjwa
MADAKTARI na wahudumu wa kimatibabu watapigwa faini ya Sh1 milioni au miaka miwili gerezani iwapo kwa kujua au kupitia utepetevu wao, watapatikana wamemdhulumu mgonjwa.
Haya yatafanyika iwapo wabunge watapitisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Afya (2024) ambao unapendekeza adhabu hiyo kali, iwe sheria.
Utepetevu au mapuuza ambayo yamewekwa katika sheria hiyo ni kufanya upasuaji vibaya, kutumia huduma za kimatibabu vibaya, kukosa kumfuatilia mgonjwa, kumpa anayeugua dawa ambazo haziendani na tatizo lake pamoja na makosa mengine yanayojitokeza kipindi cha matibabu.
“Mhudumu, mtu au ajenti wa hospitali husika ambaye atapatikana na hatia chini ya sheria hii atatozwa faini ya Sh1 milioni au kifungo cha miaka miwili au zote mbili,” ikasema msaada huo.
Adhabu hiyo pia itawaendea wahudumu wa afya wanaofichua maelezo kuhusu magonjwa ya wanaotibiwa bila idhini yao. Pia baadhi ya wahudumu ambao wana tabia ya kuwadhulumu wagonjwa wao kuwa kuwanajisi au kuwabaka pia watapitia adhabu hii kali.
Mswada huo umedhaminiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Afya Robert Pukose umetaja hospitali za umma, zile za kibinafsi, vituo vya kimatibabu na kliniki kama vituo vitakavyomulikwa.
Kwa sasa adhabu pekee kwa wahudumu wa afya ni kuondolewa kwa leseni za wahudumu wa afya. Mswada huo unakuja wakati ambapo kumekuwa na visa vingi vya madaktari na maafisa wa kliniki kuwadhulumu wagonjwa.
Wiki jana, Muungano wa Wahudumu wa Kimatibabu na Matabibu (KMPDU) uliondoa leseni ya mhudumu wa kimatibabu ambaye alipatikana akimbaka mgonjwa.
Afisa huyo wa kliniki alipatikana akimbaka mgonjwa ambaye alikuwa akisafishiwa damu. Alikamatwa na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000.