HabariSiasa

Madiwani Kiambu wafuata ulafi wa wabunge

July 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA ERIC WAINAINA

MADIWANI katika Kaunti ya Kiambu wameshangaza Wakenya kwa kutenga zaidi ya Sh100 milioni kugharimia vikao vya umma kuhusu miradi mbalimbali kwenye bajeti iliyoidhinishwa na Gavana Ferdinand Waititu.

Kwenye bajeti hiyo, bunge la kaunti limetenga jumla ya Sh1.3 bilioni kwa matumizi ya jumla ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020.

Kupitia afisi mpya iliyobuniwa ya Hazina ya Ushirikishaji wa Umma, kila diwani kati ya wawakilishi wadi 60 waliochaguliwa ametengewa Sh108,000 kila mwezi kufadhili mikutano ya umma katika afisi zao za wadi.

Hii ina maana kwamba kila diwani atapata Sh1.3 milioni kila mwaka kufadhili mikutano hiyo kulingana na bajeti hiyo.

Kisheria majukumu ya madiwani ni uwakilishi, kutunga sheria na kukosoa serikali ya kaunti inapohitajika kufanya hivyo.

Madiwani wateule, ambao idadi yao ni 32, nao hawataachwa mikono mitupu kwa kuwa watagawanya Sh14 milioni kutoka kwa Hazina ya Ushirikishaji wa umma kwa madiwani walioteuliwa.

Hii ina maana kuwa kila diwani aliyeteuliwa, ambao wengi wao ni wanawake waliopewa nyadhifa hizo ili kutimiza usawa wa kijinsia, atapokea Sh437,000 kwa mwaka.

Kwa kuwa hakuna sheria inayoruhusu matumizi hayo, maswali sasa yameibuka kuhusu uhalali wa hazina hiyo ikizingatiwa kwamba mikutano ya kushirikisha umma kuhusu maswala ya kaunti huwa haiandaliwi kila mwezi.

Hata hivyo, Kamati ya Bajeti la Bunge la Kaunti inayoongozwa na Diwani wa Kiu, Dan Ngugi na Naibu wake Nduta Muongi (mteule) walipendekeza sheria ibuniwe ya kuhalalisha matumizi hayo ili kuzima malalamishi yatakayoibuka.

Gharama ya matumizi ya kaunti pia inatarajiwa kuongezeka baada ya madiwani kujitengea Sh180 milioni kwa safari za ndani ya nchi huku Sh28.8 milioni zikitengewa kufadhili ziara zao nje ya nchi.

Dalili za matumizi haya ya kushangaza zilianza kuonekana mapema pale Karani wa bunge, Joseph Ndirangu alipofika mbele ya kamati ya kuandaa bajeti na kulalamika kwamba bunge hilo limekuwa likitengewa pesa kidogo kwenye bajeti, hali aliyodai inasababisha bunge hilo kutoweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Hatua ya madiwani wa Kiambu kijitengea kiasi kikubwa cha pesa kwenye matumizi yasiyo na umuhimu kwa wananchi, inafuata ile ya Bunge la Kitaifa ambapo wabunge wamependekeza kujiongezea mishahara kutoka Sh1.1 milioni kila mwezi hadi Sh2.9 milioni.