HabariHabari za Kitaifa

Magavana 17 wapanga mikakati ya kuepuka baridi 2027

October 30th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

HUKU uchaguzi mkuu wa Agosti 2027 ukikaribia, magavana 17 wanaokamilisha mihula yao miwili wanapanga hatua zao zinazofuata kisiasa, baadhi wakilenga viti vya useneta na wengine wakitaka nyadhifa za juu serikalini au kustaafu siasa za uchaguzi.

Hata hivyo, mipango yao huenda ikatatizwa na mswada unaopendekeza magavana wanaoondoka mamlakani wasiruhusiwe kuwania viti vya Seneti au mabunge ya kaunti hadi miaka mitano ipite.

Mswada wa Marekebisho ya Katiba wa 2026, uliowasilishwa na Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango, unalenga kuzuia viongozi hao kuingia mara moja katika taasisi zinazochunguza matumizi ya fedha na utawala wao.

Miongoni mwa magavana wanaowania viti vipya ni Ahmed Abdullahi wa Wajir, Muthomi Njuki wa Tharaka Nithi, Anne Waiguru wa Kirinyaga, Joseph ole Lenku wa Kajiado, Mutahi Kahiga wa Nyeri na Julius Malombe wa Kitui.

Bw Abdullahi ametangaza azma yake ya kuwania useneta wa Wajir, huku Bw Njuki akitaka kuendea kiti cha Seneta Mwenda Gataya, ambaye anatarajiwa kuwania ubunge.

Bi Waiguru, kwa upande wake, ametangaza nia ya kuwa Naibu Rais mwaka 2027. Alisema uzoefu wake kama mtumishi mkuu serikalini, waziri, gavana na mwenyekiti wa Baraza la Magavana unampa uwezo wa kuhudumu katika wadhifa huo.

Bw Kahiga anataka kuingia Seneti akisema uzoefu wa kuongoza kaunti kwa miaka kumi utamsaidia kutetea ugatuzi na kupinga serikali ya kitaifa kuingilia majukumu ya kaunti.

Gavana wa Kajiado, Bw Lenku anakabiliwa na changamoto baada ya kutofautiana na chama cha ODM kuhusu mipango ya kugawana nyadhifa na UDA. Amesema yuko tayari kuondoka ODM iwapo chama hicho kitaendelea kumtenga.

Baadhi ya magavana pia wanapanga kuwaunga mkono washirika wao ili waendelee kuwa na ushawishi baada ya kuondoka mamlakani.

Gavana wa Garissa, Gavana Nathif Jama anataka useneta na amemuunga mkono Seneta Abdulkadir Haji kumrithi kama gavana.

Mwenzake wa Tana River, Dhadho Godhana anataka useneta na amependekeza Mbunge wa Galole Said Hiribae kumrithi huku Gavana Hillary Barchok  wa Bomet akimuunga mkono aliyekuwa gavana Isaac Ruto kurejea katika wadhifa huo huku akilenga useneta.

Hata hivyo, si wote wanaotaka kuendelea na siasa za uchaguzi.

Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o na wa Vihiga Wilber Ottichilo wamesema hawatawania nyadhifa nyingine.

Joshua Irungu wa Laikipia bado anashauriana kuhusu kuwania useneta au kushawishi siasa akiwa nje ya Bunge.

Mswada wa Bw Murango unataka marekebisho ya Katiba na Sheria ya Uchaguzi ili magavana wanaohudumu au walioondoka mamlakani ndani ya miaka mitano kabla ya uchaguzi wazuiwe kuwania useneta na viti vya wawakilishi wa wadi katika mabunge  ya kaunti.

Seneta huyo anasema kipindi hicho kitapatia taasisi muda wa kuchunguza maswali kuhusu uongozi na matumizi ya fedha za umma bila uwezekano wa migongano ya kimaslahi.

Lakini Bw Kahiga amepinga pendekezo hilo, akisema linawadhalilisha magavana kwa kuwachukulia kana kwamba wote wameiba.

Anasisitiza kuwa kuchaguliwa kuwa seneta hakumpi gavana kinga dhidi ya kujibu maswali kuhusu uongozi wake.

Mswada huo unasubiri kusomwa mara ya pili katika Seneti, huku wanaoupinga wakisema unaweza kuwanyima magavana haki ya kushiriki uchaguzi na kuwania nyadhifa za umma.