Magavana hawakuhusishwa katika mradi wa ukodishaji wa vifaa vya matibabu – Oparanya
Na CHARLES WASONGA
MAGAVANA wamesema kuwa serikali ya kitaifa haikuwahusisha katika mpango wa ukodishaji wa vifaa vya matibabu (MES) na hivyo hawajui gharama kamili ya mradi huo.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Bw Wycliffe Oparanya hata hivyo ameambia kamati teule inayochunguza endapo madai ya matumizi mabaya ya pesa za umma katika mradi huo kwamba vifaa hivyo vilileta manufaa makubwa kwa kaunti zote 47.
“Hatujui yaliyomo kwenye kandarasi kati ya serikali kuu na mkandarasi aliyepewa zabuni ya kuwasilisha vifaa hivyo. Hii ni kwa sababu hatukuhusishwa katika hatua zote katika mpango huo tangu ulipoanzishwa mnamo 2015,” akasema Oparanya.
“Isitoshe, hatujaona kandarasi ya mradi huo ingawa vifaa vimeimarisha zaidi huduma za afya katika kaunti zetu,” akaongeza Bw Oparanya ambaye ni gavana wa Kakamega.
Alikuwa ameandamana na mwenzake wa Laikipia Ndiritu Mureithi na mawaziri kadhaa wa afya katika kaunti akiwemo Profesa Richard Muga wa Homa Bay.
Bw Oparanya aliambia wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Isiolo Fatuma Dullow kwamba magavana walilazimishwa kuunga mkono mradi huo licha ya wao kuibua maswali kuhusu namna ulivyotekelezwa.
“Ingawa mwenyekiti wetu wa zamani Isaac Ruto aliibua pingamizi kuhusu namna mradi huo ulivyokuwa ukitekelezwa, alipuuzwa. Baadhi yetu tulitia saini muafaka wa maelewano (MoU) kuhusu mradi huo chini ya shinikizo,” akasema.
Gavana Oparanya alisema Jumatano, ingawa serikali ya kitaifa hutenga Sh9.5 bilioni kwa ajili ya mradi huo, pesa hizo huwa haziwasilishwi moja kwa moja katika kaunti husika.
“Tunasikia kuwa kila kaunti imekuwa ikichangia Sh95 milioni kwa mradi huo kila mwaka na sasa mchango umeongezwa hadi Sh200 milioni. Hata hivyo, pesa hizo zimekuwa zikitolewa katika serikali kuu bila kutufikia,” akasema.
Chini ya mpango huo, hospitali mbili katika kila kaunti zilipokea vifaa na mitambo ya kisiasa ya kutibu magonjwa sugu kama vile kansa, maradhi ya figo. kisukari na maradhi ya moyo.
Mradi huo, ambao ulitarajiwa kugharimu Sh38 bilioni, ulianzishwa mnamo 2015 na serikali ya kitaifa.
Vifaa hivyo vilifaa kusambazwa na Wizara ya Afya katika hospitali zote lengwa.
Hata hivyo, bunge la seneti limeibua maswali kuhusu mradi huo likishuku kuwa huenda pesa za umma zilitumika visivyo chini ya mradi huo.
Mnamo Jumanne kaimu Msimamizi wa Bajeti (CoB) Stephen Masha aliambia kamati hiyo ya seneti kwamba tangu 2015 hadi sasa afisini yake imeidhinisha matumizi ya Sh25.9 bilioni kwa ajili ya mradi huo.
Hata hivyo, Bw Masha alisema afisi yake haikuweza kufuatilia kujua ikiwa pesa hizo zilitumika kulingana na sheria au la.
“Wajibu wa kujua ikiwa pesa hizo zilitumika ipasavyo au la ni wa Katibu wa Wizara ya Afya. Kazi ya afisi yetu ilikuwa ni kuidhinisha matumizi ya fedha ambazo tayari zilikuwa zimetengwa katika bajeti,” akasema Bw Masha.