Mahabusu watoroka jela askari wakiwa wanatazama mpira kwenye runinga
MAAFISA wa ngazi za juu wa idara ya magereza wamekita kambi katika Gereza la Wundanyi, Kaunti ya Taita Taveta kuchunguza jinsi wafungwa wanane walitoroka Jumamosi usiku.
Duru katika gereza hilo ziliambia Taifa Leo kuwa, uchunguzi utaangazia maafisa waliokuwa kazini usiku huo ili kubaini iwapo walihusika kwa vyovyote katika kutoroka kwa wanane hao.
Afisa aliyeomba kutotajwa jina kwa kuhofia adhabu alisema wakati wa kisa hicho ambacho kilisemekana kutokea saa tano na dakika 40 usiku, maafisa waliokuwa kazini walikuwa wameenda kutazama mechi ya kandanda kwenye runinga.
Wakati huo, mechi kubwa iliyokuwa ikiendelea ni ya dimba la LaLiga kati ya Real Madrid na Real Valladolid. Real Madrid ilishinda 3-0, mabao yote yakifungwa na Kylian Mbappe.
“Wafungwa wengine ndio waliwaarifu waliporejea kwamba wenzao walikuwa wametoroka. Walihofia kwamba wasipofanya hivyo, wangeadhibiwa kwa kutosema,” afisa huyo akaeleza.
Watatu kati yao walikamatwa baadaye Jumapili huku juhudi zikiendelezwa kuwatafuta watano waliosalia.
Kulingana naye, seli ilikuwa na wafungwa 37 waliokuwa wakisubiri kufikishwa mahakamani siku tofauti.
Uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa, wanane hao walikata bati ndipo wakatoroka.
Mnamo Jumapili, Kamishna Jenerali wa Magereza Patrick Aranduh alizuru gereza hilo.
Jumatatu, kikosi kingine kutoka makao makuu ya magereza na msimamizi wa magereza katika kaunti, Bw Frank Opondo, walikuwa kwenye mkutano karibu siku nzima.
Kulingana na baadhi ya wakazi wa Wundanyi, waliamshwa na ving’ora usiku wa Jumamosi bila kujua kilichokuwa kikiendelea.
Walieleza kuwa, ving’ora vilifuatwa na purukushani wakati maafisa wa magereza na polisi walipojitahidi kuchukua hatua.
“Hatukujua ni nini kilikuwa kikiendelea hadi siku iliyofuata. Tulidhani hata kulikuwa na moto. Tusingeenda huko kwa sababu ni sehemu inayolindwa,” akasema Bw Emmanuel Mwang’ombe, mmoja wa wakazi.
Kamishna wa eneo la Pwani, Bi Rhoda Onyancha, alisema maafisa wa usalama wamezidisha msako na wana matumaini kwamba wafungwa watano ambao bado wako mafichoni watapatikana.