Majangili warejelea uvamizi maeneo ya Baringo viongozi wakijipiga kifua
ZAIDI ya watu 20 wameuawa na majangili katika kaunti ndogo ya Baringo Kaskazini, Kaunti ya Baringo huku wengine 10, 000 wakitoroka makwao tangu Januari mwaka jana.
Kulingana na Kamanda wa Polisi katika kaunti hiyo, Bw Julius Kiragu, maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mashambulio ya majangili ni Barketiew, Loruk, Sibilo na Rondinin.
Kwa mfano, watu watatu waliuawa katika eneo la Loruk majuma mawili yaliyopita baada ya majangili kuvamia na kuiba ng’ombe 200 na mbuzi kadhaa.
Mmoja wa waliouawa ni Bw Musa Chemursoi, 55, aliyeuawa kwa kupigwa risasi na majangili alipokuwa akifuata ng’ombe wake walioibwa nyumbani kwake kijiji cha Riong’o.
Bw Karuga alisema serikali imeanzisha kambi za polisi katika maeneo kadhaa kama vile Kapsebeiwa, Kosile, na Yatya ili kuweka usalama na kuzuia mashambulio.
“Aidha, maafisa wa usalama wanashika doria kwa kutumia magari maalum ya kivita haswa katika wadi ya Saimo/Soi,” kamanda huyo akaongeza.
Mashambulio mengi ya majangili yamechipuza tena katika wadi ya Bartabwa na kusababisha maelfu ya wakazi kuhama makwao huku masomo yakitatizwa katika shule za msingi za Yatya, Kagir, Kosile miongoni mwa zingine.
Kando na Baringo, maeneo kadhaa ya Bonde la Kerio pia yameshuhudia mchipuko mpya wa mashambulio ya majangili hali inayoibua maswali kuhusu ufanisi wa juhudi za serikali za kurejesha utulivu maeneo hayo.
Kwa zaidi ya miezi saba tangu Mei mwaka jana, utulivu ulikuwa umerejea katika maeneo hayo kufuatia operesheni kali iliyoendeshwa na vikosi vya usalama.
Kambi za usalama zilikuwa zimeanzishwa katika maeneo ambako majangili hao hupitia wakitoroka.
Operesheni hiyo ya maafisa kutoka vitengo mbalimbali vya usalama ilianzishwa mnamo Februari 2023 katika kaunti za Baringo, Samburu, Laikipia, Turkana, West Pokot na Elgeyo Marakwet.
Maafisa waliotumika kupambana na wahalifu hao walitoka vitengo kama vile; Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Polisi wa Kupambana na Wezi wa Mifugo (ASTU), Polisi wa Kupambana na Ghasia (GSU) na Polisi wa Akiba (NPR).
Isitoshe, mnamo Machi mwaka jana, maafisa wa usalama kutoka vikosi mbalimbali walifanya mashambulio makali katika Bonde la Tandare, linalotumika kama maficho ya majangili hao katika kaunti ndogo ya Baringo Kusini.
Mashambulio mapya ya majangili pia yameripotiwa upya katika eneo la Tot katika Bonde la Kerio ambapo watu watatu waliuawa.
Waliouawa wiki jana ni wanawake wawili na mhudumu mmoja wa boda boda.Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Kerio Valley Zablon Okoyo alithibitisha kisa cha Tot, akieleza kuwa wavamizi hao sita waliiba ng’ombe 11.
“Tunasaka wavamizi hao na kwa ushirikiano na wenzetu kutoka Baringo nina imani kuwa tutawakamata,” akasema Bw Okoyo.
Aliwashauri wakazi kudumisha utulivu na kutojaribu kufanya mashambulio ya kulipisha kisasi.