Habari

Majonzi, vilio baada ya ajali ya ndege Ethiopia

March 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

MAJONZI yalitanda maeneo mbalimbali ya nchi, jamaa na marafiki wakiomboleza wapendwa wao waliofariki kwenye ajali ya ndege nchini Ethiopia, na kuwaua watu 157, wakiwemo Wakenya 32 mnamo Jumapili.

Katika kijiji cha Kwa Amos, eneobunge la Bahati katika Kaunti ya Nakuru, familia moja inaomboleza vifo vya watu watano.

Familia hiyo ya Mzee John Quindos Karanja, ilipoteza mkewe Wangui Quindos, bintiye Caroline Nduta Karanja na wajukuu Ryan Njoroge (7), Kelly Paul (5) na Ruby Pauls (miezi tisa).Watano hao walikuwa miongoni mwa Wakenya 32 waliangamia kwenye ajali iliyohusisha ndege ya kampuni ya Ethiopian Airways, iliyokuwa ikienda Nairobi kutoka mjini Addis Ababa.

Hapo jana kifaa cha kurekodi habari za safari za ndege (Black Box) kilipatikana kwenye vifusi.

“Sina amani na bado nimechanganyikiwa. Nimepoteza familia yangu. Niko Nairobi nikijaribu kufuatilia mambo hapa na pale kabla ya kurudi nyumbani hapo baadaye,” akasema Bw Karanja.

Mmoja wa majirani wake aliambia Taifa Leo kuwa, Bw Karanja alikuwa ameenda Nairobi Jumapili asubuhi kupokea familia yake iliyokuwa ikisafiri kutoka Canada, ambako mkewe amekuwa tangu mwaka jana akimtembelea bintiye.

“Mkewe Karanja alisafiri Canada mwaka uliopita kwa mwaliko wa bintiye aliyekuwa akiishi Canada pamoja na mumewe,” akasema Bw Martin Muchiri, ambaye ni rafiki wa karibu wa familia ya Bw Karanja.

Bw Karanja alikuwa ameondoka nyumbani Jumapili asubuhi kuelekea Nairobi kuwalaki wapendwa wake, kabla ya kupokea habari hizo za majonzi.

Bw Muchiri alisema walikuwa wameandaa karamu ya kukaribisha familia hiyo lakini ilipofika jioni Bw Karanja alimpigia simu akimweleza mipango yote ilikuwa imeharibika kufutia vifo vya wapendwa hao.

Mjini Homa Bay, maombolezo yalitanda katika boma ya Mzee Philip Jaboma Akeyo, ambaye bintiye Isabela Jaboma alikuwa miongoni mwa walioangamia.

Alisema alikuwa alipokea habari hizo kutoka kwa mwanawe wa kiume, Alan Onyango, aliyempigia simu kutoka Nairobi mnamo Jumapili alasiri.

Isabela, aliyekuwa na umri wa miaka 31, alikuwa akisafiri kutoka Cairo nchini Misri, alikokuwa ametumwa kikazi na shirika la Hope for Cancer Kids.

Mzee Jaboma alisema alizungumza na bintiye kwa simu mara ya mwisho wiki iliyopita alipokuwa akipanda ndege kuelekea Misri.

“Nduguye alikuwa uwanja wa Jomo Kenyatta kumpokea wakati alipofahamishwa kuwa Isabela alikuwa miongoni mwa waliofariki,” akaeleza.

Katika kaunti za Vihiga na Trans Nzoia, familia ya Cedric Galia Asiavugwa wa miaka 32, ilikuwa kwenye majonzi baada ya kupokea habari za kifo chake.

Marehemu Cendric alikuwa akirudi nyumbani kutoka mjini Washington nchini Amerika, kuhudhuria mazishi ya mmoja wa jamaa zake. Alikuwa akisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Georgetown.

Alizaliwa katika kijiji cha Luzu kilichoko Chamakanga katika Kaunti ya Vihiga, kabla ya familia yake kuhamia eneo la Mawe Tatu, Kaunti ya Trans Nzoia.

Dadake, Beatrice Achitsa alisema babake, Govedi Asiavugwa yumo Nairobi kufuatia habari hizo za kuhuzunisha alizosema zimetikisa familia yake.

Rafiki za marehemu walisema alikuwa na nia ya kuwa padre kabla ya kubadili mawazo na kusomea sheria. Amemuacha mjane na mtoto

Katika Kaunti ya Kakamega, familia ya Derick Lwugi Kivia ilikuwa ikiomboleza kifo cha mwanao wa miaka 54, waliyemtaja kama tegemeo kuu kwao.

Marehemu Lwugi, ambaye alizaliwa katika kijiji cha Naliaba eneobunge la Ikolomani, alikuwa na uraia wa Kenya na Canada.

Mamake, Elizabeth Chumazi, alisema mwanawe alikuwa ameahidi kumpeleka hospitali kwa matibabu maalum baada ya kufika Kenya.

Alisomea katika shule ya msingi ya Naliaba, Kakamega High, Chavakali High na Chuo Kikuu cha Jepun alikopata digrii ya Uhasibu.

Familia yake ilisema alikuwa akiwafadhili kimasomo wanafunzi 25 wa sekondari kutoka Kakamega na Vihiga. Amemuacha mjane na watoto watatu.

Taarifa ya Phylis Musasia, Derick Luvega, George Odiwuor and Shaban Makokha