Makurutu wasimulia walivyohongana kuingia KDF
BERNARD ROTICH na DENNIS LUBANGA
BAADHI ya makurutu walionaswa wakiwa na barua feki za kujiunga na jeshi wamekubali kwamba walitoa hongo ili kupata nafasi kwenye KDF.
Makurutu hao waliwasimulia maafisa wa kijeshi jinsi walivyotoa hongo ya Sh300,000 kila mmoja kufanikisha ndoto zao ambazo zilikatizwa baada ya kukamatwa wakiwa na barua feki za kujiunga na idara hiyo.
Maafisa wa jeshi waliwanasa zaidi ya makurutu 50 katika chuo cha mafunzo ya kijeshi mjini Eldoret waliokuwa wameripoti kujiunga na jeshi wakiwa na barua feki walizokabidhiwa na maafisa walaghai waliopokea fedha zao wakati wa usajili. Walionaswa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kukabiliwa na mashtaka mbalimbali.
Msemaji wa KDF, Kanali Paul Njuguna hata hivyo amesema kwamba idara hiyo ilikuwa imewaonya Wakenya kujihadhari na watu waliokuwa wakiwaitisha hongo ili kuwasaidia kujiunga na jeshi.
“Tulikuwa tumewaonya Wakenya kuhusu ufisadi na kuwataka kujiepusha na watu wanaotumia ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana ili kuwahadaa na kuwafilisi fedha zao,” akasema Kanali Njuguna.
Mwaathiriwa ambaye hakutaka jina lake linukuliwe alisimulia kwa masikitiko namna babake alivyotoa Sh300,000 kwa afisa wa cheo cha juu katika kituo cha jeshi cha Lanet ili kufanikisha usajili wake.
“Sehemu ya fedha hizo zililipwa kama pesa taslimu na masalio yakatumwa kupitia huduma za Mpesa ndipo tukakabidhiwa barua ya kutuwezesha kuripoti chuoni,” akasema kurutu huyo aliyelaghaiwa.
Kulingana na Kanali Njuguna, waliokamatwa walifichua kwamba walitoa zaidi ya Sh300,000 kila mmoja kabla ya kupewa barua za kuripoti kwenye kambi hiyo ya kijeshi.
Baadhi ya vijana inasemekana waliuza mali yao kama ardhi ili kupata fedha za kulipa hongo kabla ya kukabidhiwa barua hizo feki.
Makurutu waliokumbwa na sakata hiyo wanaendelea kuzuiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi mjini Eldoret wakitarajiwa kufikishwa kortini uchunguzi utakapokamilika.