HabariSiasa

Mamaye Judy Wakhungu akamatwe – Mahakama

June 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Kuamua Kesi za Ufisadi Jumanne imeamuru mama ya aliyekuwa Waziri wa Mazingira Judy Wakhungu anayeshtakiwa pamoja na Mbunge wa Sirisia John Walukhe kwa ufisadi wa Sh297milioni katika kashfa ya mahindi akamatwe na kufikishwa kortini.

Hakimu mwandamizi Bi Elizabeth Juma aliamuru Bi Grace Wakhungu ashikwe na kufikishwa kortini Juni 22, 2020 kusomewa hukumu katika kesi hiyo inayowakabili.

Bi Wakhungu hakufika kortini kupokea hukumu ya kesi hiyo, huku wakili anayemwakilisha akimweleza Bi Juma kwamba mteja wake ni mgonjwa na “hangefika kortini.”

Kiongozi wa mashtaka aliomba kibali cha kumtia nguvuni mama huyo kitolewe kwa vile hakuna ripoti kamili iliyotolewa kuhusu ugonjwa.

“Unahitaji muda kufika lini ili umlete mahakamani?” Bi Juma alimwuliza wakili anayemwakilisha.

“Naomba muda hadi Jumatatu wiki ijayo. Natumaini atakuwa amepata nafuu,” wakili alijibu.

Mahakama iliwapata na kesi ya kujibu wawili hao katika kesi hiyo ya kupokea pesa kutoka kwa Halmashauri ya Nafaka na Mazao (NCPB) wakidai walikuwa na tenda ya kuagiza kutoka ng’ambo tani 40,000 za mahindi.

Mahindi hayo yalihifadhiwa katika kampuni ya washtakiwa hao.

“Kulingana na ushahidi uliowasilishwa kortini na Tume ya Kupambana na Ufisadi nchinI, mko na kesi ya kujibu,” hakimu aliamua.

Bw Waluke alikana shtaka la kuhusika na kashfa hiyo. Anakabiliwa na shtaka la kuwasilisha kwa njia ya ufisadi Sh114,600,000 akidai zilikuwa gharama ya kuhifadhiwa mahindi hayo ya NCPB na kampuni ijulikanayo kama Chelsea Freights.

 

Mashtaka dhidi yao yanasema mnamo Machi 19, 2013 wakiwa wakurugenzi wa Erad Supplies & General Contractors pamoja na kampuni nyingine kwa jina Erad Supplies and General Contractors walifuja NCPB Sh297,386,505 wakidai ni gharama ya kuhifadhi tani 40,000 za mahindi.

Mnamo 2003, NCPB ilitangaza tenda ya kununua tani 180,000 za mahindi.

Hala General Trading LLC, Euroworld Commodities Limited na Erad ziliteuliwa kuwasilisha tani 40,000 kila moja ilhali Purma Holdings na Freba Investments zilikubaliwa kuagiza tani 30,000 za mahindi.

Mzozo ulipozuka kati ya NCPB na Erad Bw Evans Thiga aliteuliwa kusaka suluhu ndipo akaamuru Erad ilipwe Sh564 milioni zikiwa ni gharama ya kuhifadhi mahindi hayo.

NCPB ilikata rufaa katika mahakama kuu na kusikizwa na Jaji mstaafu Leonard Njagi aliyeamuru Erad isilipwe.

Erad ilikataa rufaa mbele ya majaji watatu wa mahakama hii ya upili kwa ukuu na hapo kesi yake ikatupiliwa mbali tena.

Ushahidi uliowasilishwa mahakamani ni kwamba kampuni ambayo Erad iliiomba iiuzie mahindi kutoka ng’ambi kwa jina Ropack CC International, haikuwa inahusika na biashara ya mahindi.

Kwa mujibu wa ushahidi, Erad ilikuwa iagize tani 40,000 kutoka ng’ambo lakini NCPB haikuipa stakabadhi muhimu za kuiwezesha kuagiza mahindi hayo kutoka ughaibuni.

Baadaye Erad ilipata maagizo ya kutwaa pesa katika akaunti za NCPB katika Benki ya Kenya Commercial Bank na bidhaa nyinginezo zilizo na thamani ya Sh297 milioni.

Kufuatia uchunguzi uliofanywa na Kamati ya Uwekezaji ya Bunge (PIC) uamuzi ulifikiwa Erad isilipwe pesa hizo kwa vile ilikuwa imeghushi stakabadhi ilizopeleka mahakamani kama ushahidi. Pia PIC ilisema Erad haikuwa na idhini ya kuagiza mahindi kutoka ng’ambo.

Ushahidi ulisema mnamo Februari 24 2009, Walukhe akiwa mkurugenzi wa Erad alitegemea ushahidi ghushi kudai malipo ya $1,146,000 (Sh114 milioni) katika jopo iliyosikiza mzozo huo kati ya NCPB na Erad.

Hati hiyo iliyotolewa na Erad ilikuwa itegemewe na Chelsea Freights kama ushahidi  kuwa ndiyo ilihifadhi tani 40,000 za mahindi yaliyoagizwa kutoka ng’ambo.