Mamilioni ya Ruto yagawanya makanisa
Na NDUNGU GACHANE
VIONGOZI wa makanisa wamegawanyika kuhusu mikutano ya harambee ambayo Naibu Rais William Ruto amekuwa akifanya huku wakitofautiana kuhusu iwapo wanafaa kukubali michango ya wanasiasa.
Dkt Ruto amesisitiza kuendelea na harambee makanisani ambapo amekuwa akitoa mamilioni ya pesa.
Maaskofu wa makanisa makuu nchini, kama vile, Kanisa Katoliki, Kanisa la Anglikana Nchini (ACK) na African Independent Pentecostal Churches of Africa (AIPCA) wamejipata katika njia panda baada ya kushindwa kuamua ikiwa yatazima wanasiasa kuongoza harambee katika makanisa yao au la.
Jumapili, Naibu Rais William Ruto anaongoza harambee kubwa ya kusaidia makanisa tisa katika eneobunge la Kapseret, Kaunti ya Uasin Gishu itakayohudhuriwa na wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wanaounga mkono azma yake ya kuingia Ikulu 2022.
Katika Kanisa Katoliki, Kadinali John Njue ametoa wito kwa maaskofu wake kudhibiti makanisa yao kwa kuzuia visa ambapo wanasiasa husababisha fujo katika makanisa hayo.
Kadinali Njue alisema hayo akirejelea kisa ambapo fujo zilizuka katika Kanisa Katoliki la Gitui, kaunti ya Murang’a pale Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na Mbunge Maalum Maina Kamanda walizozana hadharani kuhusu ni nani aliyepaswa kuongoza shughuli za mchango katika kanisa hilo.
“Maaskofu wanafaa kutoa ushauri maalum ili kuzuia aibu na fujo katika makanisa yetu. Mtu anayekaa chini ya mti anaelewa kile kinachoendelea nah ii ndio maana maaskofu wanapaswa kutoa mwelekeo kwa makanisa yao,” akaambia Taifa Leo kwa njia ya simu.
Na huku Askofu wa Dayosisi ya Kanisa Katoliki ya Murang’a James Maria Wainaina akizima shughuli za harambee zinazoongozwa na wanasiasa makanisani, mwenzake anayesimamia Dayosisi ya Embu Paul Kariuki amesema ataendelea kuwaalika wanasiasa, haswa Dkt Ruto, kuongoza harambee katika makanisa yake. Askofu Kariuki ametetea harambee zinazoongozwa na Ruto akisema zinachangia maendeleo sio tu makanisani bali katika jamii nzima.
Bidii kazini
Akiongea wiki jana katika Kanisa la St Paul Cathedral mjini Embu, Askofu huyo aliwalinganisa mahasidi wa Dkt Ruto na nzi ambaye huwaonea wivu nyuki kutokana na bidii yao kazini.
“Wao ni kama nzi, kazi yao ni kutafuta mahala palipooza. Kisha huanza kuambia nyuki waache kutangatanga namna ambavyo Naibu Rais huambiwa anatangatanga,” Askofu Kariuki akawaambia waumini ambao waliangua kicheko.
Ingawa Kiongozi wa ACK Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit ametangaza kuwa kanisa hilo limepiga marufuku harambee zinazoongozwa na wanasiasa katika makanisa yao baadhi ya maaskofu wa kanisa hilo wameendelea kuwaalika wanasiasa kuongoza michango katika makanisa wanayoongoza.
Baadhi ya makanisa ya ACK katika eneo la Mlima Kenya, kwa mfano, yamekuwa yakimwalika Naibu Rais William Ruto kuongoza shughuli za kuchanga fedha za kufadhili miradi mbalimbali.
“Ingawa tunatambua wajibu unaotekelezwa na moyo wa harambee katika maendeleo ya jamii yetu, Kanisa la Kianglikana linatafakari kupiga marufuku mtindo wa wanasiasa kuongoza harambee ndani ya makanisa yake. Ikiwa ni Wakristo na wanasiasa wanataka kufanya harambee wafanye hivyo nje ya majengo ya Kanisa,” Ole Sapit alisema mnamo Aprili mwaka huu.
Amri ya Ole Sapit ilizingatiwa na Askofu Julius Karanu wa Dayosisi ya Murang’a Kusini ambaye amepiga marafuku harambee zozote zinazoongozwa na wanasiasa katika makanisa yaliyoko chini ya usimamizi wake.
Hata hivyo, Askofu Joel Waweru na Timothy Gichere wa Dayosisi za Nairobi na Mlima Kenya ya Kati, mtawalia, wameendelea kuwaalika wanasiasa katika makanisa yao.
Huku Askofu Waweru akibashiri kuwa Dkt Ruto atashinda katika uchaguzi mkuu wa 2022, Gichere ameshikilia kuwa kanisa halina uwezo wa kutofautisha a pesa chafu au zile safi, hatua ambayo imeandelea kugawanya kanisa hilo.
Katika Rift Valley baadhi ya makanisa la Kiprotestanti yamelalamikia Dkt Ruto huongoza harambee katika makanisa ya maeneo mengine na kuwapuuza. Viongozi wao walisema wao pia wangetaka kupata sehemu ya pesa hizo.
“Je, Rift Valley haina makanisa ambayo Dkt Ruto anaweza kuzuru? Tuko na shule, makanisa ya kujengwa na watoto masikini wanaohitaji kusaidiwa,” kiongozi mmoja wa kanisa alimwambia Dkt Ruto.
Inaonekana kwamba Naibu Rais ameitikia wito huo na kesho yuko katika ngome yake ya Uasin Gishu kuongoza harambee kusaidia makanisa tisa katika eneo bunge la Kapseret linawakilishwa na Bw Oscar Sudi. Wabunge, maseneta, magavana na madiwani wapatao 100 wanatarajiwa kuhudhuria shughuli hiyo.