Mapengo katika dili ya Ruto na Trump
ZIARA ya Rais William Ruto nchini Amerika wiki hii imezaa mikataba mikubwa ya ufadhili na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, lakini pia imeanika hatari na changamoto za hadhi mpya ya Kenya katika mkakati wa Washington barani Afrika.
Ziara hiyo inaweza kuingia katika historia kama mojawapo ya safari muhimu zaidi za kigeni za utawala wake, ikifungua upya mfumo wa usaidizi wa Amerika, kuleta makubaliano makubwa ya fedha, na kuiweka Kenya katika ajenda ya Amerika barani Afrika.
Hata hivyo, imeonyesha changamoto mpya katika diplomasia ya kiuchumi, ikiwemo uzingatiaji wa masharti, ushindani wa mataifa makubwa, na shinikizo kwa Kenya kuthibitisha uwezo wa usimamizi katika mpango mpya wa ufadhili wa moja kwa moja.
Rais Ruto ni kiongozi wa kwanza wa Afrika kupata ziara ya kiserikali Amerika enzi ya Rais Joe Biden, na sasa ndiye wa kwanza pia kusaini mfumo mkubwa wa ushirikiano wa maendeleo chini ya utawala wa Rais Donald Trump.
Kiini cha ziara hiyo kilikuwa makubaliano mapya ya afya ya thamani ya Sh323 bilioni, yanayofafanua upya ushirikiano wa miaka 25 kati ya mataifa hayo mawili, huku Kenya ikiwa nchi ya kwanza kunufaika na mfumo mpya wa ufadhili wa afya wa Amerika baada ya mageuzi ya USAID.
“Huu ni ufadhili wa ruzuku, unaopunguza mzigo kwa Kenya katika kipindi ambacho mataifa mengi yanakabiliwa na madeni,” asema msemaji wa Ikullu Hussein Mohamed.
Anasisitiza kuwa mkataba huo ni ishara ya imani ya Amerika katika mageuzi ya Kenya na unaendana moja kwa moja na ajenda ya bima ya afya kwa wote (UHC).
Kwa mara ya kwanza, fedha za afya kutoka Amerika zitaelekezwa moja kwa moja kwa mifumo ya Serikali ya Kenya, yakiwa mabadiliko makubwa kwani hapo awali zililetwa nchini kupitia mashirika yasiyo ya serikali.
Wakosoaji wanasema mfumo wa zamani ulifanya takriban asilimia 40 tu ya fedha kufika kwa wahudumu.
Hata hivyo, mfumo wa moja kwa moja unakuja na mzigo: Kenya lazima ithibitishe uwazi, uwezo wa usimamizi na kuepuka dosari hususan katika KEMSA, vinginevyo ufadhili unaweza kusitishwa.
Rais Ruto pia alipata makubaliano ya kihistoria ya kubadilisha deni la Sh129.3 bilioni kuwa uwekezaji wa utoshelevu wa chakula ikiwa ni mpango wa kwanza wa aina yake kuidhinishwa na Trump.
Hakukuwa na hatua ya maana kuhusu kuongeza muda wa makubaliano ya kibiashara ya AGOA, suala muhimu kwa wauzaji wa bidhaa Kenya.
Pia, kulikuwa na mwelekeo mdogo kuhusu ufadhili wa usalama licha ya nafasi ya Kenya katika uthabiti wa kikanda.
Na kwa kuwa siasa za Amerika zimegawanyika mno, baadhi ya makubaliano yanaweza kukumbana na pingamizi katika bunge au mahakamani.
Mnamo Aprili, makubaliano kati ya Rais Ruto na Rais Xi Jinping wa China yalizua ghadhabu Amerika.
Sasa, haijulikani China itachukuliaje mikataba mipya ya mabilioni kati ya Kenya na Amerika.
Hata hivyo. Prof David Monda, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Amerika, anaonya kuwa Kenya inakabiliwa na hatari za kisheria, siasa za kieneo na za usalama wa data kutokana na muafaka huu mpya.
Anahoji kuhusu usalama wa data ya afya ya Wakenya katika mfumo unaofadhiliwa na Amerika.
“Ni sheria gani itatumika kulinda data hii? Sheria ya Amerika, Kenya au sheria za kimataifa?” anauliza.
Bila mifumo madhubuti ya ulinzi, anaonya Kenya inaweza kupoteza udhibiti wa data muhimu za kiafya.
Prof Monda pia anaonya kuwa makubaliano yanaakisi “msimamo wa Trump” ambao ni wa kubadilika-badilika na wa kibiashara zaidi kuliko ya ushirikiano.
“Siku moja anaunga mkono, siku inayofuata anageuka,” anasema, akionya kwamba Kenya inaweza kupata shida kupanga sera za muda mrefu.Anasema Rais Ruto sasa yuko katikati ya misimamo miwili tofauti—ule wa Biden wa ushirikiano wa kimataifa, na ule wa Trump wa kupendelea Amerika kwanza.
Prof Monda anaonya kuwa China inaweza kutafsiri hatua za Kenya kama kupendelea Amerika, hasa ikizingatiwa kwamba Beijing ndiyo imefadhili miradi mikubwa zaidi ya miundomsingi nchini.
Hali hiyo, asema, inaweza kuchochea mabadiliko katika jinsi China inavyotoa mikopo, kuwekeza au hata kushirikiana na Kenya.