Maseneta wataka watoto wasiokuwa na makao wapewe nyumba nafuu za serikali
MASENETA sasa wanaitaka serikali kuu ishughulike idadi ya juu ya watoto na watu ambao hawana makao kabla ya kukimbilia kufunga makao ya watoto.
Wiki jana, serikali ilitangaza kuwa itafunga makao ya watoto mayatima na wale ambao wametelekezwa yanayoendeshwa na watu binafsi.
Ilisema baada ya kufunga makao hayo, itakumbatia mbinu bora zaidi ya kuwaangalia watoto hao.
Serikali inalenga kukumbatia mageuzi kupitia Baraza la Kitaifa la Huduma za Watoto ambalo linalenga kuanzisha malezi ya kifamilia na jamii.
Seneta Maalum Esther Okenyuri ameutaka utawala wa Rais William Ruto utafakari kuanzisha makazi salama zaidi kwa watoto na makundi mengi yaliyotelekezwa.
“Je wizara ya Leba na Maslahi ya Kijamii kwa ushirikiano na washikadau imetekeleza sera pana ya kitaifa ili kuhakikisha watoto wasiokuwa na makao pamoja na akina mama wanapata njia ya kujikimu?”akauliza Bi Okenyuri.
Seneta huyo wa ODM alitaka ushirikiano kati ya wadau wote ili kubaini nini hasa kimekuwa kikisababisha idadi ya watoto wa kurandaranda mitaani kuongezeka ndipo kuwe na mbinu muafaka ya kupambana na suala hilo kabisa.
Ushirikiano huo kwa mujibu wa kiongozi huyo unastahili kushirikisha serikali za kaunti, idara ya kuangazia maslahi na haki za watoto, idara ya utoaji nasaha, mafunzo na afya kwa makundi yaliyotengwa.
“Kamati ya Leba ya Seneti inastahili kutuambia iwapo kuna mgao wa kutosha kwenye bajeti ili kujenga, kuajiri wafanyakazi na kuimarisha utoaji wa huduma bora pamoja na makao mazuri,” akaongeza.
Seneta wa Murang’a Joe Nyutu alisema serikali haifai kumakinikia tu suluhu bali pia ishughulikie kinachosababisha watoto na hata watu wazima kukosa makao.
Bw Nyutu hata alipendekeza serikali itenge baadhi nyumba za gharama nafuu ambazo ujenzi wao umekamilishwa, kuwapa watoto na akina mama.
“Hizi ni changamoto za zamani na kumekuwa na jaribio la kuwapa makao watoto mijini lakini kumekuwa na upinzani mkali. Nyumba zinazojengwa kupitia ushuru wa Wakenya zinastahili kutumika kuwapa watoto hawa makao,” akasema Bw Nyutu.
Seneta wa Kisii Richard Onyonka alisema kuwa serikali haijali maslahi ya watoto na hata watu wazima kwa sababu baadhi wamekuwa wakiishi barabarani kwa kipindi kirefu.
“Ukienda miji mbalimbali utawapata watoto barabarani. Naunga mkono wito kuwa wapewe makao kwenye nyumba ambazo zinajengwa na serikali,” akasema Bw Onyonka.
Naye Seneta Maalum Miraj Abdillahi alisema watoto wasiokuwa na makao wamegeuka kero Mombasa huku tabia zao zikiathiri shughuli za kitalii.
“Wanajifanya vibaya mbele ya watalii na kusawiri Mombasa kama jiji la ombaomba. Serikali isake mbinu ya kuwapa makao,” akasema Seneta Abdillahi.