HabariSiasa

Matiang'i atabomoa mafia wa mihadarati?

August 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

WAZIRI wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i anakabiliwa na moja ya vita vikali zaidi tangu alipoteuliwa waziri 2013 katika kupambana na walanguzi wa dawa za kulevya na magenge ya uhalifu.

Dkt Matiang’i ameibuka kuwa waziri anayetenda anayosema. Lakini sasa anatazamwa na wengi kuona kama ndiye atakayefanikiwa kuu joka la biashara ya dawa za kulevya hasa Pwani.

Watangulizi wake waliojaribu kukabiliana na biashara hiyo haramu walilemewa kutokana na uwezo mkubwa wa kifedha wa wahusika, uhusiano wao na wakuu ndani ya idara za usalama, mahakama, wanasiasa, maafisa wa ngazi za juu serikalini na kimataifa.

Walanguzi hao huzua hofu hata katika mataifa makubwa kama Amerika kutokana na ukatili na uwezo wao wa kifedha.Ishara kuwa waziri huyo mkakamavu anafahamu hatari inayomkodolea macho ilijitokeza wiki iliyopita aliposema: “Hatuwezi kuacha maisha ya vijana wetu yawe mikononi mwa wahalifu, hata kama wana ushawishi kiasi gani katika jamii au kisiasa. Sisi si wapumbavu na tunaelewa hatari zinazohusishwa na ulanguzi wa mihadarati. Lakini hatutalegeza kamba kwani lazima tulinde maisha ya vijana wetu na kudumisha usalama wa kitaifa.”

Kando na mihadarati, wizara ya Dkt Matiang’i pia inaendesha operesheni Mombasa kupambana na magenge ya wahalifu, ambayo kulingana naye yana uhusiano na wanasiasa na walanguzi wa dawa za kulevya.

Kabla ya kuanzisha operesheni hizo ambazo zinalenga kunasa watu wenye ushawishi kisiasa na kibiashara wanaofadhili uhalifu Pwani, Dkt Matiang’i alikuwa tayari amechukiza wengi wa matabaka ya juu.

Mapema mwaka huu, baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa kitaifa hawakuficha hasira zao wakati waziri huyo alipoanzisha msako wa kupambana na bidhaa ghushi zinazohatarisha maisha ya binadamu.

Hii ni kutokana na kuwa operesheni hiyo dhidi ya bidhaa ghushi iliathiri mno uagizaji bidhaa kutoka nchi za kigeni, ilhali baadhi ya wawekezaji wa biashara hizo wanaoaminika kuwa matapeli ni wanasiasa na washirika wao.

Baadaye, alianzisha mapambano makali kukabiliana na ukiukaji sheria katika makampuni ya uchezaji kamari.

Katika sekta hii, wawekezaji na wasimamizi hasa wa makampuni makubwa ya kamari huwa ni washirika wa wanasiasa tajika kitaifa.

Endapo atafanikiwa katika operesheni hizi, Dkt Matiang’i atakuwa ameendelea kuweka historia kama kiongozi aliyetembea bila viatu kwenye makaa moto na kushinda.

Hii ni licha ya kuwa kuna wakosoaji wanaosema wakati mwingine huwa hajali kuhusu sheria wala maagizo ya mahakama kuhusu hatua anazochukua.

Alipokuwa akisimamia Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), waziri huyo aliweka mapambano makali dhidi ya vyombo vya habari hadi akahakikisha sheria ya kuhamia mfumo wa upeperushaji kidijitali ulitekelezwa.

Mtindo huu wake wa kutumia kila mbinu kuafikia malengo yake ulishuhudiwa zaidi alipokuwa katika Wizara ya Elimu.

Ni wakati huo ambapo mabadiliko makubwa yalionekana katika wizara hiyo hasa kuhusu usimamizi wa mitihani ya kitaifa na usambazaji vitabu kwa shule za umma.

Kwa upande mwingine, mashirika ya uchapishaji vitabu bado hulalamika hadi leo kuhusu hasara wanayopata baada ya Wizara ya Elimu kubadilisha mtindo wa usambazaji vitabu kwa shule za umma.

Hata hivyo kuna vita ambavyo Dkt Matiang’i bado hajafaulu kushinda. Mwaka jana alitangaza msako mkubwa wa kulainisha sekta ya matatu na hata akahusika yeye binafsi. Lakini sekta hiyo bado imejaa fujo na ukiukaji mkubwa wa sheria.

Vita dhidi ya watengenezaji na wauzaji bidhaa feki navyo viligonga mwamba kwani bidhaa hizo zingali zimejaa kwenye maduka.