Habari

Matiang'i azuru Eastleigh kuwatuliza wakazi

May 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imekanusha madai kuwa amri kufungwa kwa mtaa wa Eastleigh ilitolewa kwa nia ya kuwaadhibu wakazi.

Akiongea Jumamosi alipozuru mtaa huo, Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i alitaja madai hayo yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa eneo hilo kama propaganda zisizo na msingi wowote.

Dkt Matiang’i aliwaambia wazee na viongozi wa chama cha wafanyabiashara wa Eastleigh kwamba amri hiyo iliwekwa baada ya mtaa huo kuandikisha visa vingi zaidi vya maambukizi ya corona.

“Rais amenituma hapa kuwahakikishia watu wa Eastleigh na raia wote wa Jamhuri ya Kenya, kwamba sisi ni sehemu ya familia moja kubwa. Kwa hivyo, mtu asiseme kwamba kwa kufunga sehemu hii au ile tunalenga kuumiza jamii fulani,” akasema.

Dkt Matiang’i alikuwa ameandamana na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Nairobi Esther Passaris.

Waziri pia alikariri kuwa amri hiyo inalenga kuwakinga wakazi dhidi ya maradhi ya Covid-19 ambayo kufikia sasa yamesababisha vifo vya watu 30.

Visa vilivyothibitishwa kufikia jana Jumamosi ni 649.

“Sielewi ni kwa ni mtu anazunguka akidai kuwa sisi kama serikali tunawabagua. Iweje kwamba tuwabague ilhali nyie ndio huajiri idadi ya raia na hulipa kiwango kikubwa cha ushuru kupitia biashara zenu? Ushuru mnaolipa ndio huchangia kuendesha shughuli katika idara mbalimbali za serikali,” akasema.

“Huu ni ni wakati wa sisi sote kushirikiana kupambana na jinamizi hili. Sio wakati wa kueneza propaganda. Sote ni Wakenya na huwa tunaumia tukipoteza hata mtu mmoja,” Dkt Matiang’i akaongeza.

Eneo la Eastleigh lina maduka makubwa ya kuuza nguo na bidhaa nyinginezo kutoka mataifa ya ng’ambo.

Eneo hilo pia lina mikahawa na vituo vingi vya kubadilisha sarafu za kigeni.

Mnamo Jumatano Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitangaza amri ya watu kutoingia na kutoondoka katika mtaa wa Eastleigh na eneo la Mji wa Kale Mombasa ili kuzuia kuenea kwa Covid-19.

Baada ya kutolewa kwa amri wakazi wa Eastleigh waliibua malalamishi wakidai hatua hiyo itawaathiri zaidi biashara zao zikifungwa.